31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TMA: MVUA ZA MASIKA KUTIKISA

Na MAULI MUYENJWA-DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza kuanza kwa mvua za masika na kutahadharisha mamlaka za miji kuweka sawa miundombinu ya kupitisha maji ili kuondoa uwezekano wa kutokea mafuriko ambayo yanaweza kuathiri jamii.

Kutokana na hilo, TMA imezishauri Mamlaka ya Maafa na wadau wengine kuchukuwa hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira, mipango na kujiandaa kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na mwenendo wa mvua.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mamlaka hizo na wananchi wanashauriwa kuhakikisha wanajiandaa kwa kuweka sawa mindombinu inayowazunguka ili kujihakikishia usalama wakati wa mvua za masika ambazo zinatarajiwa kuwa kubwa katika baadhi ya mikoa.

“Kutokana na uwezekano wa vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa, tunashauri mifumo na njia za kupitishia maji kufanya kazi sawa na hatua hizo zichukuliwe hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kwa sababu vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza,” alisema Dk. Kijazi na kuongeza.

 “Kutokana na uhaba wa maji salama unaotarajiwa kwa shughuli za binadamu, ikiwamo usafi, wananchi wanashauriwa kuchukua hatua stahiki kuzuia milipuko ya magonjwa,” alisema Dk. Kijazi.

Aidha mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kutoakana na hali ya ukame ulioyakumba maeneo mengi ya nchi, sasa yanaweza kupata mvua, hivyo wanatakiwa kupata ushauri wa maofisa kilimo kujiandaa kwa kilimo.

“Maeneo ya kusini na pwani ya kusini ambayo ni mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Lindi ambako mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa,” alisema Dk. Kijazi.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini unatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani, vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko hafifu wa mvua katika baadhi ya maeneo hayo,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kijazi, mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku Nyanda za Juu Kusini zikitazamiwa kuwa na mvua za wastani au chini ya hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles