*Mbowe, Lowassa waonja machungu ya polisi, Vijana kadhaa wakamatwa
VERONICA ROMWALD Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Singida Mashariki , Tundu Lissu (Chadema), jana alihojiwa kwa zaidi ya saa tano na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.
Lissu ambaye pia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi saa 7:46 jana mchana akitokea Kituo cha Polisi Dodoma.
Ilikuwa ni safari iliyoanzia mkoani Singida ambako alitiwa mbaroni juzi baada ya kumaliza mkutano wake jimboni kwake.
Taarifa za kukamatwa kwa Lissu na polisi mkoani Singida zilienea juzi kupitia ujumbe uliosambazwa kwenye mitandao ya jamii, ambao ulitolewa na Lissu na baadaye kuthibitisha na Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, jana alithibitisha kukamatwa kwa Lissu kwa kile alichoeleza kuwa alitoa maneno ya uchochezi katika mkutano wake wa hadhara jimboni kwake.
Sedoyeka alisema Agosti 3 mwaka huu saa 9:45 alasiri Lissu, alifanya mkutano halali wa hadhara mjini Ikungi ambako alidai alitoa maneno ya uchochezi.
“Katika mkutano huo mbunge huyo alitoa maneno ya uchochezi kwamba Septemba mosi watu wote wajitokeze kufanya mikutano kuunga kaulimbiu ya kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), na kwamba Rais Magufuli hana mamlaka ya kuwazuia kwa sababu jukumu hilo ni la Mkuu wa Polisi wa Wilaya,” alisema Sedoyeka.
Alisema baada ya mkutano kumalizika mbunge huyo alikamatwa na polisi kwa madai ya kutoa lugha ya uchochezi na kufunguliwa jalada namba CD/IR/5962/2016 katika Kituo Kikuu cha Polisi.
ALIYESAMBAZA UJUMBE ASAKWA
Sedoyeka pia ametangaza kumsaka mtu aliyesambaza ujumbe ambao amaedai “una ishara zote za uchochezi” unaoonyesha umeandikwa na Lissu baada ya kukamatwa na jeshi hilo.
Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya jamii kuhusu ujumbe huo.
Ujumbe huo ambao pia umenukuliwa na jeshi hilo katika taarifa yake, ulieleza jinsi polisi mkoani Singida walivyomkamata Lissu baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara huku akihamasisha watu kutokubali kunyamazishwa na “Udikteta Uchwara”.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya jamii kuhusu ujumbe mfupi wa maneno uliosambazwa katika mitandao hiyo baada ya kukamatwa kwa Lissu ukiwa na ishara zote za uchochezi…,” alisema Sedeyoka na kuongeza:
“Katika uchunguzi huo endapo mtu yeyote atabainika kutuma taarifa hiyo basi Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za sheria zinazostahili ikiwamo kumkamata na kuwafikisha mahakamani mara moja.”
Ujumbe huo ulisomeka, “Wakubwa sana salamu. Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini ya ulinzi wa polisi Singida. Nimemaliza kuhutubia mkutano wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya jimbo la Singida Mashariki.
“Mara baada ya kushuka jukwaani nilifuatwa na RCO wa mkoa aliyejitambulisha kwa jina la Babu Mollel na kuniarifu kuwa ameelezwa na RPC nikamatwe. Wakati huohuo, kuna amri ya kunikamata iliyotoka Dar es Salaam kwa hiyo nipo nguvuni ninasubiri maelekezo ya wanapotaka kunipeleka…
“Its likely (kuna uwezekano) nitasafirishwa Dar usiku huu. Infact ni usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa ‘there is no turning back’ (hakuna kurudi nyuma), there is no shutting up (hakuna kufunga mdomo). Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote nitakapokuwa.
“Whether in freedom or in jail as long as I have a voice to speak with. (Nikiwa huru au kifungoni ilimradi nina sauti ya kuzungumza) sitakubali kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Msikubali kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Aluta continua!!!! From Tundu Lissu”.
Kamanda Sedoyeka alisema endapo itathibitishwa kuwa Lissu ndiye aliyeandika na kusambaza ujumbe huo ataingia tena matatani kwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za sheria kama lilivyoeleza jeshi hilo.
Hiyo ni mra ya tatu kukamtwa kwa mbunge huyo kwa kipindi cha miezi michache na amekwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za uchochezi.
Kesi ya kwanza ni ile iliyodaiwa ametoa lugha ya uchochezi katika habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio na kesi ya pili ni ya kutoa maneno ya uchochezi kwa kumwita Rais Magufuli ‘Dikteta Uchwara’
ILIVYOKUWA DAR JANA
Mapema asubuhi kabla kiongozi huyo wa Chadema hajafikishwa kituoni hapo, baadhi ya madiwani na wenyeviti wa Chadema walikuwa wamekwisha kuwasili kwenye eneo hilo Kituo Kikuu cha Polisi.
Saa 7:45 gari namba T 312 CWM lenye vioo vyeusi liliwasili katika eneo hilo likiwa limembeba Lissu ambaye alikuwa na maofisa wa polisi.
Baada ya kushuka katika gari hilo, Lissu alionyesha alama ya vidole viwili juu kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa pembeni mwa kituoni hapo, ambao waliitiia kwa sauti baada ya Lissu kusema ‘Peoples’ nao wakaitikia ‘Power’
“Giza haliwezi kulishinda nuru, daima nuru itang’aa gizani…. Waache wamkamate kila mara maana wanazidi kumpaisha tu, leo tunakaa hapa hadi kieleweke,” walisikika wakisema wafuasi hao katika eneo hilo la polisi
Wakati wote mahojiano hayo yakiendelea, askari walisimama kila upande kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Saa 9:40 alasiri, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili kituoni hapo na gari namba T. 830 DEW lakini alijikuta akigonga mwamba kumuona Lissu baada ya kuzuiwa na askari kuingia katika eneo hilo na kulazimika kuegesha gari lake pembeni.
LOWASSA NA MACHUNGU
Ilipotimu saa 12: 15 jioni, Waziri Mkuu wa zamani ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na Vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa naye aliwasili kituoni hapo na gari namba T 771 DEA.
Alipofika kituoni hapo, alikwenda alipokuwa Mbowe na viongozi wengine wa Chadema akiwamo Meya wa Kinondoni ,Boniface Jacob huku wafuasi wa chama hicho waliokuwapo kituoni hapo wakishangilia: “Rais..rais….rais…”
Baada ya muda mfupi askari waliongezwa huku watu waliokuwa wakishangilia wakawa wanafukuzwa kutoka eneo la kituo hicho na askari mmoja alisikika akisema kwa sauti kuwa ‘mkusanyiko huo si halali’.
Katika kufukuzana huko, kijana mmoja ambaye hakuweza kufahamika jina lake mara moja, alikamatwa na askari hao na kuingizwa ndani ya kituo hicho.
Punde, gari la maji ya kuwasha liliwasili na kuegeshwa katika lango la kuingilia kituoni hapo na baadaye liliondoka na kuanza kuzunguka mitaa inayozunguka kituo hicho.
Saa 12:50, Mbowe na Lowassa waliingia katika magari yao na kuondoka kituoni hapo huku ulinzi ukiimarishwa zaidi kwa kuletwa askari wenye bunduki za zisasi za moto.
KAULI YA KIBATALA
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala, alisema Lissu ameshikiliwa kwa tuhuma za kutoa lugha ya uchochezi na kwamba wanatarajia kesho (leo) atafikishwa mahakamani.
“Walimkamata Ikungi Singida wakamleta hadi Dodoma akalala selo Chamwino na kusafirishwa usiku hadi Dar es Salaam saa 7.00 mchanatulimpa chakula na saa 9.00 mahojiano yalianza hadi saa 12.00 jioni,” alisema Kibatala na kuongeza:
“Kwa kuwa mteja wetu wameshamshikilia kwa saa 24 tunatarajia kesho watampandisha kizimbani kumsomea shtaka lake”.
Pamoja na Kibatala mawakili wengine waliokuwapo polisi ni Wakili John Mallya na Omari Msemo.