24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Abiria wenye akili kama madereva wao kukiona

Waendesha bodaboda wakiwa katika maandamano.Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

UKURASA wetu huu wa Vituko vya Bodaboda tumekuwa tukiutumia vyema kukumbushana baadhi ya mambo lakini wadau wote wanatakiwa kufahamu vituko si kwa madereva tu hata abiria wanaotumia usafiri huo wamejaa vituko.

Madereva wamekuwa wakiushangaza umma pale wanapoelimishwa kutumia kofia ngumu kwa usalama wao wenyewe wanakaidi kana kwamba wanawakomoa askari wa usalama barabarani.

Wamekuwa wakipata ajali na kuumia vibaya lakini bado wanabishana na ukweli kwamba utaratibu wa kuvaa kofia ngumu ni kwa faida yao na abiria aliyebebwa.

Hakuna asiyefahamu kwamba vijana wanavichwa vigumu hawataki kufuata taratibu za uendeshaji salama wa chombo hicho.

Pamoja na kufahamu hilo, bado abiria anayepakiwa katika bodaboda hapewi kofia ngumu lakini anakubali kusafiri hivyo hivyo, akipata ajali akaumia anamlalamikia dereva kwamba alikuwa mwendo kasi.

Hakumbuki kwamba safari yake haikuwa salama tangu alipoianza na hakuliona hilo kwamba linaweza kuwa na madhara makubwa endapo atapata ajali.

Wanawake wameonekana kuwa na sababu nyingi za kugomea kuvaa kofia hiyo ngumu, miongoni mwa sababu hizo ni uchafu wa kofia hiyo na wengine wanashindwa kuivaa juu ya nywele zao nzuri walizotengeneza kwa gharama kubwa, wakihofia kuziharibu.

Sababu ya uchafu inawezekana kuwa ya msingi isipokuwa kuna njia ya kuepukana na uchafu huo ikiwamo kuvaa mfuko laini kabla ya kofia hiyo.

Wale wanaokataa kwa sababu ya kuharibu nywele, hoja zao hazina msingi kwa kuwa nywele hizo haziwezi kuzuia kuumia inapotokea ajali.

Lakini wadau wanashauri kama wanawake wanaweza kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya kwenda navyo saluni kwanini wasianzishe utaratibu wa kununua kofia ngumu kwa ajili ya matumizi yake anapohitaji kupanda pikipiki.

Ushauri huo unawezekana kwa sababau gharama ya kofia hiyo si kubwa ukilinganisha na madhara yanayoweza kutokea kwa kutoivaa.

Askari wa usalama barabarani wamejitahidi kwa hali na mali kutoa elimu lakini imekuwa vigumu kueleweka, hadi sasa wamefikia uamuzi wa kumkamata dereva na abiria ambao watakutwa hawajavaa kofia hiyo.

Wanasema dereva na abiria wote wataadhibiwa na dereva hawezi kuachiwa na Polisi hadi anunue kofia hiyo.

Madereva wanachukulia kuzoea hiyo hali ndio maana hawabadiliki, lakini abiria kuna haja ya kubadilika, kujali usalama kwa kuhakikisha hawezi kupanda bodaboda bila kuwa na kofia hiyo.

Ni uhuru wa mteja kuamua apande bodaboda ipi hivyo kama dereva uliyemzoea hana kofia ngumu ya kukupa unatakiwa kuchukua uamuzi mgumu wa kumwacha na kutafuta mwingine anayezingatia sheria za barabarani.

Abiria wanasababisha matatizo mengi kwa kutojali, wapo wanaopanda katika vyombo hivyo akiwa na watoto watatu, wawili anakuwa nao mshikaki na mwingine mmoja anamweka mbele kwa dereva anakali tangi la mafuta.

Tubadilike wanawake hayo si mazingira salama kwa watoto, inapotokea ajali uzembe unakuwa umeanzia kwako.

Nampongeza Mkuu wa Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga kwa kufikia uamuzi wa kuwabana abiria wanaotumia usafiri huo kwani bila hivyo hilo somo halitaeleweka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles