KATIKA kusafiri na kona nyingi, kuna mabaya na mazuri huwa najiuliza kwanini wenzetu wameweza kufika hapo walipo na kuweza kuendeleza jamii zao. Kwanini kila wakati utakuta tunakwamishana na badala ya kuendeleza wengi wapate faida unakuta ubinafsi unatawala nafsi zetu. Hivi ni mila na desturi ambazo zinafanya tuwe hivyo?
Ni vibaya kufikiria kwamba ni Watanzania tu ambao tupo hivyo lakini utakuta ni wengi na wapo katika kila jamii. Sasa kwanini hizi jamii zingine zimeweza kujiendeleza na kufika kwenye kiwango ambacho ni cha juu sana. Je, tumekosa misingi mizuri ya maendeleo? Misingi ambayo tungeweza kujenga mambo mengi ya kimaendeleo.
Naamini katika kuendeleza jamii zetu ni muhimu kwamba kuwe na nidhamu na watu ambao wanajitolea bila ya kujali nani anafaidika. Kama kuna miundombinu ambayo inatufanya sisi wote tuweze kutengeneza msumari kwa nidhamu na kuufikisha kwenye soko kwa wakati unaotakiwa basi tumelewa majukmu yetu na nini kinatakiwa.
Sasa, ni kitu gani kinatuzuia sisi tusifike hapo? Tunakosa nini kingine ukitoa nidhamu. Maana yake nidhamu sio shina la matatizo. Tukiangalia ndani sana utafikiria labda ni elimu na elimu utawezaje kupaa bila nidhamu ya kuweza kufundisha au nidhamu ya kupenda kufundisha.
Kitu kikubwa sana katika jamii nyingi ni imani na imani inaleta nidhamu ya kufundisha na kufundisha inaleta elimu kwa wengi. Sasa hapa katikati kuna kitu ambacho tumekipoteza. Imani unazikuta zipo nyingi lakini huwezi ukakuta imani ambayo inakwenda ndani sana katika jamii au ina historia ndefu ambapo imeweza kuendeleza na kuwa ni falsafa ambayo inaunganisha na kuleta maendeleo ya mwili na roho.
Katika mfumo huo utaona kwamba kwa kujaribu kuunganisha hizo sehemu ya kueleza, kufahamu na kuweza kuweka katika mazingira ambayo yanaeleweka na kuweza kuwapa ufahamu mkubwa na ikawa sehemu ya maisha ya jamii na watu binafsi utakuta jamii inaigiza na kuingiza kiunganishi ambacho hakina urefu au upana ambao umetoka katika hiyo jamii.
Katika kuigiza basi utakuta mengi mazuri na mengine mabovu yanachukuliwa bila ya kufahamu chanzo cha huo ubaya au uzuri. Kama ni fikira ambazo hazijazaliwa na hiyo jamii basi kuelewa kunakuwa sio wa kina na jamii inakuwa na misngi ambayo sio madhubuti.
Kuigiza falsafa ambayo haina misingi au chanzo kutoka katika jamii yako mara nyingi inaingiza pia makosa na matatizo ambayo pole pole yataitafuna jamii kwa ndani kama kansa. Sasa kama hii ni chombo ambacho unataka kuleta maendeleo ya kijamii basi hii pia italeka vikwazo katika jamii. Unaiga vitu ambavyo havina uhalisi na jamii yako pamoja pia kuzaliwa, kulelewa na kukuzwa katika mazingira ya hapo kwenu.
Hicho chombo ndicho kinachotumika katika kuleta elimu na baadaye kuleta maendeleo. Ni mashua ambayo inapokelewa katika bandari zote na kuleta bidhaa za uhakika. Chombo hicho kinaunganisha jamii zote na kuwawezesha wanajamii kuelewa na kutekeleza mawazo ya kimaendeleo na kuwa na upeo wa mbali.
Fikra za wanajamii zinapata changamoto ambayo inawafanya waweke jitihada kubwa kutekeleza yale matakwa ya kimaendeleo ambayo uongozi wa kijamii umeuona.
Kuelewa utamaduni wa jamii nyingine kutokana na mazingira ambayo wanajamii wamekulia, migogoro ya kisiasa na migogoro ya binaadamu huletwa hasa na kuwa na vyanzo tofauti vya falsafa. Yote hii inaweza kusababishwa pia na kutokuelewa lugha iliyotumika katika mazingira yaliyopo na uigizaji wa falsfa za wengine ambazo hazina chanzo cha shina la kijamii hapo ulipo.
Migogoro ya binadamu inaweza kuwa kutokana na kutokufahamu na kuelewa kile kinachoelezewa kwa sababu ya maneno machache tu ambayo yana maana machache tofauti kwenye lugha au tani, tabia, sentensi na au utamaduni wa lugha.
Sasa katika kuleta elimu kwa falsafa ambayo haina shina kubwa katika jamii ni mwanzo wa kutawaliwa kilugha na kimawazo. Ukijaribu kuwaelezea jamii: tutengeneze msumari au tuelimishe watu waweze kuwafundisha wengine na kuleta maendeleo, kuhifadhi na kuboresha maarifa kwa kizazi kinachofuata wengi hawataelewa ni kwa kasi gani kwani ukasi haupo kwenye hiyo jamii, au ziwe za rangi gani na pia rangi zinaweza ku2wa hazina umuhimu sana kwenye hiyo jamii.
Hizizote ni moja za changamoto nyingi ambazo jamii zetu zinakabiliwa ziwe nje au ndani ya nchi.
Leo tupo watu karibu milioni 45, tunakimbilia milioni 50. Pande hizi tupo zaidi ya milioni 180 kwa wenzetu ni soko kubwa lenye mahitaji mengi sana kuanzia mafuta ya kujipaka mpaka kutengeneza jusi na kuweka kwenye pakti tofauti. Ni kitu gani haya maendeleo hayajafika kwa haraka? Tuna kila kitu, ni kwa sababu gani tunashindwa kuona kwamba hapa fursa za kujiajiri na kuweza kuleta maendeleo kwenye jamii ni kubwa sana?
Imani, hatuna imani na uwezo wetu kwa ajili lugha na fikra tunazotumia ni za kuazima.
Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga..