23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vyombo vya habari viturejeshee ‘filamu’ ya Escrow

waandishi-wa-habari-wakiwa-kaziniNA HASSAN DAUDI

HAKUNA ubishi kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa jamii yoyote kupiga hatua kuelekea kwenye mabadiliko chanya. Mbali na kutoa taarifa, vyombo vya habari vina dhima ya kuelimisha ambayo ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo ya watu wa jamii fulani.

Iko wazi kuwa vyombo vya habari vina nguvu kubwa katika kuamua kile ambacho watumiaji wake (audience) wanatakiwa kukizungumzia.

Kupitia nadharia ya Agenda Setting, wataalamu wanadai kuwa magazeti, vituo vya redio na televisheni, ambazo ndizo njia kuu na za kuaminika za mawasiliano, huamua kulipa umuhimu jambo fulani ambalo mwishowe hugeuka ‘kauli mbiu’ kwa jamii nzima.

Kwa kuiripoti mara kadhaa habari fulani, jamii huamini kuwa ina umuhimu mkubwa kwao na hatimaye hujikuta ikiizungumzia kila uchwao.

Itakumbukwa kuwa kuna kipindi habari za mauaji ya albino ziliteka sehemu kubwa ya mazungumzo ya vijiweni, hiyo ilitokana na kupewa umuhimu mkubwa katika njia hizo za mawasiliano.

Itakumbukwa kuwa mbali na mauaji hayo ya kikatili, nadharia hii ya Agenda Setting pia iliwahi pia kushuhudiwa wakati wa mchakato wa Katiba mpya, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, ambapo vyombo vya habari viliwafanya Watanzania wote kuzungumzia mambo hayo.

Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari vinatakiwa kuwa makini katika kutengeneza ajenda kwa kuzipa kipaumbele taarifa zenye masilahi mapana kwa jamii yake.

Mwaka jana, wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa madarakani, moja kati ya kashfa zilizoibuka na kuchafua utawala wake ilikuwa ni ile ya Tegeta Escrow.

Katika hilo, vigogo kadhaa wa serikali yake walitajwa kujiingizia mabilioni ya fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Baada ya ukimya wa muda mrefu, mwezi uliopita sakata hilo liliibuka upya na kuwa gumzo kwenye vyombo vya habari.

Kilichofufua mjadala huo ni kitendo cha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).

ICSID iliyopo jijini Washington DC, Marekani, ililitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong kiasi cha Sh bilioni 320.

Lakini pia, mbali na kiasi hicho cha fedha, Tanesco waliambiwa kuwa wanatakiwa kuilipa benki hiyo riba ya asilimia nne.

Wakati skendo hiyo ikitawala vyombo vya habari na hatimaye kufufuka upya kwenye vichwa vya Watanzania wengi, viongozi wakubwa hasa wale waliohusika moja kwa moja kupiga yale mabilioni, wakaanza kuumia kimya kimya.

Hata hivyo, wakati vyombo vya habari vikiendelea kuuweka bayana ‘mchongo’ huo, mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, ukaibuka.

Kwa kutotambua umuhimu wa mjadala wa Escrow ambao kwa kiasi kikubwa unahusisha masilahi ya umma, vyombo vya habari navyo vikajikuta vimehamia kwenye vita ya Lipumba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kwa takribani wiki tatu sasa, sehemu kubwa ya vichwa habari hapa nchini imetawaliwa na kile kinachoendelea kati ya msomi huyo wa taaluma ya uchumi na CUF. Kwa lugha nyepesi, unaweza kusema vyombo vya habari vimeshafunga ule mjadala wa Escrow.

Naomba nieleweke vizuri, simaanishi kuwa sekeseke la Lipumba kuvuliwa uanachama na CUF halikupaswa kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari, lakini ilikuwa sahihi kuiacha ile ya Escrow? Nani asiyejua kuwa skendo ya kashfa imebeba masilahi mapana ya taifa kuliko suala la Lipumba na CUF? Iko hivyo.

Kwa tathimini ya haraka ambayo haihitaji elimu ya kiwango cha juu, suala la Escrow lilikuwa na uzito wa kipekee kwa sababu liliwagusa wananchi wote huku lile la Lipumba likiwagusa wanachama na wafuasi wa CUF?

Kwa lugha ya taaluma ya uandishi, kitendo hicho cha kuhamisha matukio katika jamii, vyombo vya habari kinaelezewa katika nadharia ya Spinning.

Wataalamu wa nadharia hiyo wanadai kuwa, mbali na kuamua nini watumiaji wake wanatakiwa kukizungumzia, vyombo vya habari vina uwezo mkubwa wa kuhamisha tukio lililopo vichwani mwa wengi na kuleta jipya ambalo nalo baada ya muda mfupi litakuwa na umaarufu mkubwa.

Ni ngumu kuepuka Spinning, lakini uhamaji kutoka tukio moja kwenda jingine lazima uzingatie umuhimu wa habari zenyewe. Kama wasingekurupuka na badala yake kupima uzito wa habari zote mbili, basi wangebaki na ajenda yao ya Escrow.

Lakini, ni zaidi ya ‘wendawazimu’ kuacha habari inayoonekana kuwa na faida kwa jamii nzima na kukimbilia ile inayowahusu watu wachache, huo unaweza kutajwa kuwa ni ‘usaliti’ wa masilahi ya wengi.

Ndicho kilichofanyika, bila kujua, waandishi wa habari wamelifunika suala la Escrow ambalo lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa taifa, hasa ikizingatiwa kuwa fedha zilizotafunwa na wajanja wachache zilitokana na kodi za walalahoi na kukimbilia kile kinachowahusu zaidi wanachama wa CUF ambao hawafiki hata nusu ya Watanzania wote.

Unaweza kujiuliza, vyombo vya habari vilitumia mantiki gani kulipa uzito jambo hilo lililowahusu zaidi wana-CUF na kuwaacha mafisadi wa Escrow wakipumua?

Ikumbukwe kuwa Watanzania ni wasahaulifu mno kuwatoa kwenye Escrow kwa takribani wiki tatu sasa, ni sawa na kulifuta kabisa suala hilo vichwani mwao. Je, kwa kufanya hivyo, vyombo vya habari havijawakatili?

Kama nilivyosema hapo awali, kuwa vyombo vya habari ni nyenzo muhimu ya maendeleo, lazima viwekeze nguvu kubwa katika kuhakikisha misingi ya habari zao inalenga katika ustawi wa jamii inayovizunguka.

Katika hilo, ajenda za vyombo vya habari zisivutwe na mihemko ya kisiasa na badala yake zijikite katika kuwasaidia wananchi kufahamu na njia za kutatua matatizo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles