31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Damian: Mwandishi New Habari atakayeripoti ‘Live’ uchaguzi Marekani

justins-photoAtawakilisha Wanahabari wote wa Tanzania

NA MWANDISHI WETU

NOVEMBA 8, mwaka huu, macho na masikio ya dunia ya ulimwengu yataelekezwa nchini Marekani. Siku hiyo, ni siku ambayo Taifa hilo kubwa duniani na lenye uchumi mkubwa kupita mataifa yote duniani litakuwa linafanya uchaguzi mkuu ambapo Rais wa 45 anatarajiwa kupatikana.

Katika Uchaguzi huo Mwandishi wa Kampuni ya New Habari (2006), Ltd, Justin Damian ameteuliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kuripoti uchaguzi huo baada ya kushinda shindano lililoandaliwa kumtafuta mwanahabari atakayewakilisha Tanzania kwa upande wa vyombo vya habari vya magazeti.

Swali. Kwanza kabisa hongera kwa kupata fursa hii adimu na pili unaweza kueleza kwa kifupi ulivyoweza kuipata?

JIBU: Nashukuru kwa pongezi. Programu hii ni fursa niliyoipata katika mazingira ya kiushindani. Ilitangazwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini kupitia tovuti yake ambapo waandishi wa habari wa magazeti, luninga, redio na blogu waliopenda kushiriki walitakiwa kutuma maombi yao kwa njia ya barua pepe. Kabla sijaliona tangazo la programu hiyo bosi wangu Shermarx Ngahemera alikuwa wa kwanza kuliona nakumbuka alinisisitiza kutuma maombi. Kutokana na majukumu mengi, nilijikuta nikianza kujibu maswali ambayo ni sehemu ya maombi nakuishia kati kati na nikaja kukumbuka tena siku ya mwisho kabisa. Kwa bahati nzuri, nilikuwa nimeshaanza kufanya maombi na nilifanikiwa kutuma kwa barua pepe siku hiyo.

Kesho yake nilijibiwa na ubalozi kuwa maombi yangu yalikuwa yamepokelewa na wale watakaofanikiwa kuingia raundi ya pili ndiyo watafahamishwa na kwa bahati nzuri nlifanikiwa kuvuka na kuingia raundi ya pili. Katika mchujo wa mwisho tulikuwa waandishi saba, watatu wa magazeti na wane walikuwa wa luninga.

Baada ya usaili wa mwisho uliohusisha maafisa wa ubalozi wa Marekani na walimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tulifanikiwa kupita waandishi watatu, mmoja kutoka TBC I wa pili kutoka Capital tv na mimi nikiwa mwandishi pekee wa magazeti.

Swali: unadhani ni kwa nini umechaguliwa wewe na waandishi wengine wengi waliomba wakaachwa?

Jibu: Siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja na kusema sababu fulani ndiyo iliyonifanya nichaguliwe. Kama nilivyoeleza hapo awali, programu hii ilikuwa ya ushindani na ni wazi kuwa nilikidhi vigezo kwa uhakika zaidi kuliko walioachwa na ndiyo maana nikachaguliwa.

Sababu nyingine mahsusi inawezekana ni kwa kuwa nimekuwa nikiandika uchambuzi wa maswala mbali mbali ya kisiasa kupitia kolamu yangu ya kila Jumatano inayojulikana kama Jicho la Mtanzania jambo linaonyesha mapenzi katika masuala ya siasa. Kingine ni kuwa, moja kati ya vigezo katika programu hii ni mwandishi anayechaguliwa aweze kuripoti kwa ajili ya chumba cha habari mwenyeji (host media) nchini Marekani .

Ili kuripoti kwa chumba cha habari mwenyeji ni lazima uwe na uwezo wa kuzungumza na kuandika Kiingereza lugha inayotumika nchini Marekani. Niliweza kukidhi kigezo hiki muhimu kwa kuwa nimeandikia gazeti la The African ambalo ni gazeti la Kiingereza kwa muda mrefu.

Swali: Kampeni za uchaguzi mkuu wa Marekani hasa katika ngazi ya urais mwaka huu zimekuwa na msisimko mkubwa ukilinganisha na miaka mingine, hili linaweza kuwa limesababishwa na nini? Jibu: Tofauti na miaka mingine, kampeni za mwaka huu zimekuwa za msisimko wa kipekee.

Ni kwa mara ya kwanza mgombea mwanamke Hilary Clinton kutoka moja ya vyama vikubwa yaani Democrat ameteuliwa kuwania nafasi hiyo nyeti . Kwa upande wa wapinzani wa Democrat kwa maana ya Republican, mgombea ambaye hakuwahi kujihusisha na siasa na mfanyabiashara billionea Donald Trump aliteuliwa na chama chake kugombea nafasi ya urais.

Kampeni za wagombea hawa wawili ambao wanaweka historia ya pekee katika siasa za Marekani zimetawaliwa kurushiana shutuma nzito na kauli tata ambazo hazikuzoeleka sana katika siasa za nchi hiyo. Kauli ambazo amekuwa akitoa Trump kama zenye mwelekeo wa kibaguzi, msimamo wake juu ya Waislamu, nchi za Kiafrika, unyanyasaji wa kijinsia, uhasimu wake kwa Watu wa Mexico na Watu asili ya Hispania na nyinginezo zimezua mijadala mikubwa siyo tu kwa Marekani bali duniani kwa ujumla.

Pamoja na utata huo Trump mwishowe aliwashinda wengine na kupewa nafasi ya kupeperushaa bendera kupitia chama chake.

Swali: Unakwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuripoti uchaguzi mkuu, wasomaji wako wategemee nini?

Jibu: Wasomaji wategemee kupata habari moto moto moja kwa moja kutoka viwanja vya kampeni nchini Marekani. Baada ya kufika Marekani, tutakuwa na semina ya siku mbili jijini Washington Makao Makuu ya Kituo cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari (International Centre For Journalists) kwa ajili ya kutujengea uwezo juu ya taratibu, sheria na kanuni za uchaguzi wa Marekani.

Baaada ya hapo, tutakwenda katika miji mbali mbali ambako tutafanya kazi ya kuripoti. Mimi nitakuwa katika chumba cha habari cha gazeti la Citizen Times katika mji wenye milima wa North Carolina ambako pamoja na kuripoti kwa ajili ya gazeti mwenyeji, nitaripoti kwa magazeti ya hapa nyumbani, wasomaji wakae mkao wa kula.

Swali. Ni nini matarajio yako katika programu hii?

Jibu: Nikiwa kama mwandishi anayechipukia kwanza kabisa najisikia furaha kubwa kupata nafasi hii ambayo wengi walikuwa wakiitamani.

Nimekuwa nikiandika masuala ya kisiasa kwa kipindi kidogo na safari ya Marekani kushuhudia na kuripoti uchaguzi itakuwa ni nafasi ya kujifunza namna nchi zilizoendelea kama Marekani zinavyoendesha demokrasia hasa wakati wa uchaguzi.

Ili mtu uweze kuandika au kusema jambo lenye mashiko ni muhimu kuwa na sehemu ya kuonyesha tofauti kati ya jambo moja dhidi ya jambo lingine (reference point) Unapozungumzia demokrasia ya nchi kama Marekani unazungumzia demokrasia ya miaka mingi na iliyokomaa.

Binafsi naamini yapo mambo mengi ambayo Tanzania inaweza kujifunza juu ya demokrasia na uchaguzi wa Marekani ambayo naweza kuwaletea wasomaji kwa sabau nitakuwa nimeyashuhudia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,581FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles