Na Lilian Lundo – MAELEZO
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametawataka Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anapoendelea kukiandika kitabu cha awamu ya Sita.
Waziri Nape ameyasema hayo, jana Machi 18, 2022 alipokuwa akitoa hotuba yake kama mgeni rasmi wa kongamano la kurasa 365 za Mama, ambalo liliandaliwa na Clouds Media Group na kufanyika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Nimpongeze Mhe. Rais kwa kumaliza siku 365, kwani sio kazi ndogo. Katika siku zake 365 bila wasiwasi kaendeleza yaliyofanywa na awamu Tano zilizopita na amerekebisha baadhi ya mambo ambayo yalihitaji kurekebishwa ili mambo yaende sawa,” alisema Nape.
Aliendelea kusema kuwa, kwenye kufanya marekebisho wakati mwingine unaweza kugusa hapa na pale, na ukagusa maslahi ya watu, watu wakaumia lakini ni kwa lengo jema.
“Wote kwa pamoja tuliofurahi na tulioguswa, tumuombee Rais Samia aweze kuongoza nchi yetu vizuri. Tumuunge mkono aendelee kukiandika kitabu cha awamu ya Sita,” alisisitiza Nape.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa katika siku 365 za Rais Samia ameona mwanga mkubwa katika sekta ya Habari.
“Siku 365 za Rais Samia, ni siku zilizokuwa na mafanikio, tulikuwa tunahitaji kufanya kazi kwa uhuru na sasa uhuru upo. Wajibu wetu ni kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru bila kubugudhiwa,” alifafanua Msigwa.
Aidha alisema kuwa, serikali imeanzisha mjadala wa Sheria ya huduma za Habari ya Mwaka 2016 pamoja na wadau wa habari ili kuhakikisha vitu vyote vinavyoleta vikwazo kwa waandishi wa habari katika sheria hiyo vinafanyiwa kazi.
Msigwa ameeleza kuwa, Wakati Rais Samia anaingia madarakani kulikuwa na redio 119, magazeti 270 na Online TV 552 lakini mpaka sasa kuna jumla ya redio 210 magazeti 284 na Online TV 664. Amesema kuwa, serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya vyombo hivyo vya habari kuendelea kukua.
Naye Mhariri wa Clouds Media Group na Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe, amesema katika siku 365 za Rais Samia, vyombo vya habari vimepumua, “Kwa sasa naweza kusema kalamu zetu zipo huru kufanya kazi lakini kwa kuzingatia sheria na kanuni ambazo zimewekwa,” alifafanua Joyce.
Rais Samia Suluhu Hassan, leo Machi 19, 2022 anatimiza mwaka Mmoja tangu ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021 akiwa ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki.