25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Mbarawa azindua bodi mpya TPA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameipa

 maelekezo matano Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku akisisitiza endapo yakifanyiwa kazi kwa usahihi  taasisi hiyo, itapiga hatua katika utekelezaji wa majukumu yake na kuleta tija inayokusudiwa.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizindua Bodi hiyo mpya jijini Dar es Salaam huku akiitaka kusimamia utendaji kazi katika masoko, manunuzi , uhandisi na mifumo.

Profesa Mbarawa amesema Serikali ina imani kubwa na bodi hiyo, inayoongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Balozi  Ernest Mangu aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Bodi iliyopita ilivunjwa kwa sababu mamlaka ya uteuzi ilikosa imani na utendaji kazi wake ikiwemo kuendelea kulea ubovu wa TPA hivyo Wajumbe wote tambueni mna majukumu makubwa na imani yangu kwenu ni kuhakikisha mnafanya vizuri ili kuleta matokeo chanya ndani ya TPA,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Katika maelezo yake, Profesa Mbarawa alitolea mfano utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam, akisema bado haujafikia kiwango kinachotakiwa, licha ya mizigo na meli zinazopakua mizigo kuongezeka kwa nyakati tofauti.

“Hakuna sababu ya msingi ya mchakato wa kupakua mizigo kuchukua muda mrefu kati ya siku 20 hadi 30, hili jambo linatakiwa kufanyiwa kazi haswa. Suala hili likisimamiwa vema litapunguza msongamano wa meli zinazoingia na kutoka”, amebainisha.

Ameitaka Bodi hiyo iangalie utendaji kazi wa mtoa huduma mwenza wa TPA ambao hauridhishi na kuitaka TPA ifikishe malengo iliyojiwekea ya kukusanya mapato zaidi.

Katika mkutano huo, Profesa Mbarawa alivitaja vitengo vya idara ya manunuzi na masoko, akisema bado havijatekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akiitaka bodi hiyo mpya kuangalia sekta hizo kwa jicho la tatu.

Amebainisha kuwa lipo soko kubwa DRC (Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo), hivyo  TPA ikijipanga vizuri itanufaika na soko hilo na hivyo kuleta tija.

Aidha, kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi, Ernest Mangu akizungumza amesema watajitahidi kufanyakazi kwa bidii ili kufikia lengo.

“Yapo matarajio makubwa yanayotarajiwa na Serikali kutoka kwetu, tunakuhakikisha haya matarajio tutayafikia. Serikali inaingalia bandari kwa jicho la pekee, naomba mtoe ushirikiano wa kutosha ili tutekeleze majukumu kama inavyopaswa” amesisitiza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamis ameishukuru Serikali kwa ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyotumika katika shughuli za kila siku za taasisi hiyo ikiwemo vifaa vya kushushia mizigo vilivyonunuliwa ndani ya miezi 10 na kuahidi kuvisimamia kikamilifu ili vipunguze msongamano.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka katika maeneo ya barabara ya Kilwa (Uhasibu) na Chang’ombe na kuagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Profesa Mbarawa alimtaka mkandarasi anayetekeleza miradi hiyo, kuhakikisha anakamilisha upande mmoja wa barabara ili kuruhusu magari kupita upande mmoja ifikapo Mei mwaka huu ili  kupunguza msongamano wa magari kwa watumiaji wa barabara hizo, hasa wakati  ujenzi ukiendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles