Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WATANZANIA wameshauriwa kutumia bidhaa zenye nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuepukana na vyakula vinavyozalishwa bila sifa kwa matumizi ya binadamu.
Ushauri huo umetolewa jana na Meneja wa Shirika la Chef Asili Co.LTD la mkoani Dodoma, Lupyana Chegula, alipokuwa akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kuhusiana na bidhaa zinazotegenezwa na kuuzwa bila viwango kwa watumiaji.
Alisema kuwa, kutokana na Serikali kuhamia mkoani Dodoma, Watanzania wanatakiwa kuchukua tahadhari juu ya bidhaa zinazotengenezwa kwenye viwanda ambazo havina vigezo vya TBS.
“Kwa kuwa Serikali imehamishia makao ya nchi hapa Dodoma, ni muhimu wakazi wakajiepusha na bidhaa ambazo hazina nembo ya TBS ili kulinda afya zao.
“Kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa viwanda vya kienyeji ambavyo havitambuliwi na TBS kwa kuwa kuna watu wengi hapa Dodoma,” alisema Chengula.
Pamoja na hayo, Chengula aliwataka wafanyakazi waliopewa dhamana ya kuwahudumia watu, waache tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajitume ili kuweza kujiongezea kipato.
“Fanyeni kazi zenu kwa bidii na kwa ubunifu ili muendane na kasi Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikisisitiza kila Mtanzania kuwajibika kwenye eneo lake.
“Ili kwenda na kasi hiyo, ni muhimu Watanzania wakafanya kazi kwa bidii na ubunifu ambao utawafanya kulitawala soko la ajira ambalo hivi sasa wageni wa kutoka nje ya nchi wanalimiliki,” alisema Chengula.