25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

TUKIO LA TORRES LINGEKUWA AFRIKA TUNGESEMA MENGINE

NA BADI MCHOMOLO


DESEMBA mwaka jana soka la Tanzania lilipata pigo kubwa kwa kuondokewa na mchezaji chipukizi wa klabu ya vijana chini ya miaka 20 kutoka Mbao FC, Ismail Mrisho.

Mchezaji huyo alifariki uwanjani baada ya kugongana kwa hali ya kawaida na mchezaji mwenzake na kumsababishia kifo.

Kifo chake kiliwashangaza wengi, kwa kuwa tukio lenyewe halikuwa la kutisha hadi mchezaji huyo anapoteza maisha, hata wachezaji wenzake walichukulia jambo la kawaida, hivyo walichelewa kutoa huduma kwa mwenzao.

Wengi walidhani kuwa mchezaji huyo amepata maumivu ya kawaida, wapo ambao walikwenda pembeni kwa ajili ya kunywa maji, huku wakiamini kuwa mchezaji mwenzao anapewa huduma, na waliposhituka hali ya mchezaji huyo ilikuwa mbaya na kisha kupoteza maisha uwanjani hapo hapo.

Baadhi ya wachezaji walikimbilia kumvua viatu huku wakiamini ndio huduma ya kwanza kwa mtu mwenye hali kama hiyo, kumbe walitakiwa kuwahi na kuutanua mdomo wake.

Ni wazi kwamba siku zote kifo kinatokana na mipango ya Mungu, hata kama kukiwa na huduma bora kwa kiasi kikubwa kama Mungu amepanga upoteze maisha basi hakuna namna ambayo inaweza kufanyika ili kuokoa maisha.

Lakini siku zote huduma sahihi ina mchango mkubwa wa kusaidia maisha ya mtu kwa muda fulani, ila kwa barani Afrika bado inaonekana ni tatizo kubwa viwanjani.

Juni 2003, soka la nchini Cameroon na Afrika kwa ujumla lilipata pigo kama hilo ambalo lilitokea mwaka jana nchini Tanzania, ambapo wao walimpoteza nyota wao, Marc-Vivien Foe, baada ya kuanguka uwanjani.

Mchezaji huyo ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Man City na West Ham, alipoteza maisha akiwa na timu yake ya Taifa baada ya kuanguka katikati ya uwanja kwenye kipindi cha pili cha mchezo dhidi Colombia.

Yeye hakugongana na mchezaji yeyote, lakini alianguka mwenyewe akiwa anatembea na kisha kupoteza maisha huku akipewa matibabu, hakuna ambaye ataweza kulisahau tukio hilo kwa wale wote ambao walishuhudia.

Katikati ya wiki iliyopita katika Ligi Kuu ya nchini Hispania, La Liga, kulitokea tukio ambalo lilitaka kuacha historia katika ulimwengu wa soka baada ya nyota wa klabu ya Atletico Madrid, Fernando Torres, kupoteza fahamu kutokana na kugongana kichwa na mchezaji wa Deportivo, Alex Bergantinos.

Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1, Torres alilazimika kukimbizwa hospitalini baada ya hali yake kuwa mbaya.

Torres alipoteza fahamu akiwa juu baada ya kugongana na Bergantinos, lakini wachezaji wa Atletico Madrid walimuwahi mchezaji huyo na kumpa huduma ya kwanza kabla ya madaktari kuingia uwanjani hapo.

Wachezaji wanne wa Atletico Madrid waliwahi kwenye tukio hilo wakishirikiana na mchezaji mmoja wa Deportivo kuhakikisha wanaokoa maisha ya mchezaji huyo.

Alikuwa katika hatari ya kupoteza maisha endapo wachezaji hao wangechukulia kuwa ni jambo la kawaida na kuchelewa kufika eneo la tukio, maana mchezaji huyo alikuwa anaanza kutaka kumeza ulimi wake.

Inasemekana kuwa tukio kama hilo likitokea uwanjani mchezaji anaweza kupoteza maisha mapema kama ataung’ata ulimi wake na kuumeza, lakini kama atawahiwa kwa kutanuliwa mdomo na kupewa huduma nyingine anakuwa na asilimia kubwa ya kupona.

Hicho ndicho kilichotokea kwa Torres, wachezaji waliwahi kutoa huduma huku kiungo wa klabu hiyo ya Atletico Madrid, Gabriel Arenas ‘Gabi’ aking’atwa meno na Torres wakati akipambana kuokoa maisha ya mchezaji huyo.

Gabi alikuwa wa kwanza kumshika Torres na kumtanua mdomo ili asimeze ulimi wake na ndipo mchezaji huyo aling’atwa meno na kupata maumivu, lakini aliendelea kufanya hivyo hadi madaktari walipofika eneo husika.

Ni wazi jambo kama hilo la Torres lingetokea barani Afrika chochote kingeweza kutokea, kungekuwa na uwezekano wa kumkosa mchezaji hiyo na kama si hali kuendelea kuwa mbaya kutokana na ucheleweshwaji wa huduma.

Lakini tangu tukio hilo litokee usiku wa Alhamisi na mchezaji huyo kukimbizwa hospitalini, hali yake inaendelea vizuri na tayari aliruhusiwa kurudi nyumbani siku inayofuata.

“Ninawashukuru wale wote ambao walikuwa wananiombea mara baada ya kupoteza fahamu, ninamshakuru Mungu ninaendelea vizuri na ninawatoa wasiwasi kwamba muda mfupi ujao nitarudi uwanjani.

“Wengi walikuwa na wasiwasi na hali yangu, lakini kwa sasa nipo nyumbani chini ya uangalizi wa madaktari, asanteni sana,” alisema Torres.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles