27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Tuhuma za ngono vyuoni zisipuuzwe

NA SARAH MOSSI

 SIKU kadha azilizopita vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilisheheni taarifa za kuwepo rushwa ya ngono katika Chuo Kikuu Dar es Dar es Salaam (UDSM) zilizoibuliwa na Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk. Vicensia Shule ambazo kwa kiasi kikubwa zilitikisa jamii yetu na kufanya uongozi wa chuo kukaa vikao mbalimbali kuzijadili tuhuma hizo.

Katika akaunti yake ya Twitter, Dk. Shule alionesha kusikitishwa kuwasilisha malalamiko yake juu ya tuhuma za ngono mbele ya Rais Dk. John Magufuli alipokwenda kuzindua maabara kubwa ya kwanza Tanzania ambayo pia ni ya tatu Afrika iliyopo Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Katika andiko lake, Dk. Shule alimweleza Rais kwamba kutokana na ulinzi mkali uliokuwapo siku hiyo ameshindwa kumsogelea angalau Rais apate nafasi ya kulisoma bango la malalamiko aliloandaa linalomuomba Rais afuatilie kwa karibu kilio cha wanafunzi wa kike wa UDSM kinachoeleza wanavyo athiriwa na ngono na kwa kiasi kikubwa kinarudisha nyuma malengo yao.

Nichukue nafasi hii kumpongeza Dk. Shule kwa ujasiri alioonesha angalau kuthubutu kuweka wazi madhila yanayo wasibu wanafunzi wa kike UDSM, lakini pia nimpe pole iwapo kama alipata kikwazo chochote baada ya kuweka wazi kilio hicho kwani Wahenga walinena; “Mti wenye matunda ndio wenye kupopolewa kwa mawe”

Tuhuma za ngono kwa wanafunzi wa kike kwenye vyuo vikuu nchini haziku anza leo lakini pia hazi wasibu wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam pekee, hili tatizo lipo kwenye vyuo vyote na nitamke wazi linarudisha nyuma sana malengo ya wanafunzi wa kike kwani baadhi yao wale wasiojiweza sana wamejikuta wakiingia kwenye mtego huo bila kupenda, lakini wengine hujikuta wakiondolewa vyuoni kwa visa tu ilhali wakiwa hawakutimiza malengo yao.

Sio kweli kwamba wanafunzi wa kike uwezo wao kichwani ni mdogo, wapo wanawake wengi wenye uwezo wa kielimu kuliko hata wanafunzi wa kiume, lakini asilimia kubwa hujikuta wanawekewa vikwazo kuendelea mbele kutokana na kulazimishwa kufanya ngono na baadhi ya wahadhiri wenye tamaa.

Baadhi wa kishindwa kukwamishwa kwa rushwa ya fedha, basi hukwamishwa kwa kutumia kikwazo cha ngono. Na hapa sihitaji kuelezea kwa kirefu namna ambavyo baadhi ya wahadhiri wamekuwa wakifanya kosa hilo kubwa kwa vijana wa kike waliopitia vyuoni watakuwa wamenielewa.

Mmoja wa wanafunzi katika chuo kikuu fulani hapa nchini (jina nalihifadhi) aliwahi kuzungumza nami akilalamikia tatizo la rushwa ya ngono lilivyokuwa kubwa kwenye chuo hicho, pamoja na kuripotiwa kwa uongozi wa chuo lakini mara nyingi wanaoripoti hutakiwa kupeleka ushahidi ambao pengine kwa wakati huo walalamikaji hukosa ushahidi na hivyo malalamiko yao yakionekana ni ya kuharibu sifa ya chuo ama yamhusika anayelalamikiwa.

Mwanafunzi huyo aliwahi kunieleza alipoitwa na mmoja wa wahadhiri ambaye alitaka afanye naye mapenzi kwa ahadi kuwa kwa kufanya hivyo ataweza kufaulu masomo yake lakini kwa ushujaa alikataa kufanya hivyo na kuripoti tuhuma hizo kwa uongoziwa wanafunzi na baadaye malalamiko hayo yakafikishwa kwa uongozi wa chuo ambao ulitaka atoe ushahidi iwapo kweli yalikuwapo mazungumzo hayo kati ya mhadhirina mwanafunzi.

Jambo la ajabu ni kwamba uongozi wa chuo ulimweleza mwanafunzi kwamba iwapo kweli yalikuwapo mazungumzo hayo ambayo mwanafunzi hakukubaliana nayo basi angetumia mbinu ya kurekodi mazungumzo hayo na kuyafikisha yakiwa kama ushahidi.

Sasa hapo unajiuliza, wakati mwanafunzi akiitwa na mhadhiri kuelezwa matakwa yake, hakujiandaa kama ataelezwa upuuzi huo, alijua anaitwa kwa mazungumzo ya kawaida kama ambavyo hutokea kati ya mhadhiri na mwanafunzi wake, je, huo muda waku rekodi hayo mazungumzo unatoka wapi?

Huu ni mfano mmoja wa kukwamisha malalamiko ya rushwa ya ngono yasifanyiwe kazi kwa kuweka vizingiti kwa mlalamikaji asiendelee kulalamika.

Mwanafunzi kama huyu ambaye amepeleka malalamiko yake anawekwa kwenye nafasi gani yakuendelea kimasomo na kukamilisha ndoto zake?

Bila shaka mhadhiri anayelalamikiwa anaposikia kwamba upuuzi wake umekwenda kwenye ngazi husika atafanya kila njia kumkwamisha mwanafunzi na hapo ndipo unakuwa mwisho wa mwanafunzi.

Lakini pia yapo malalamiko kwamba wapo wanafunzi wa kike hushawishi wahadhiri kufanya nao ngono, hili linaweza kuwapo kwa asilimia ndogo sana. Na hii hutokea kwa wale wanafunzi ambao hufikiri kwa kufanya hivyo ndiyo njia ya wao kutoka kielimu.

Lakini hawa ndiyo wale wanapokuja kwenye ajira wanakuwa mzigo kwa Taifa, kwani uwezo wao wa ubunifu unakuwa ni wa kiwango cha chini kabisa.

Natoa wito kwa wahusika, hususani wizara husika kufuatilia kwa karibu malalamiko hayo yenye lengo la kuharibu taswira ya vyuo vyetu, lakini pia kuwatisha wazazi walio na vijana wa kike walio vyuoni na wale wenye lengo la kufika elimu ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles