BODI ya Tumbaku Tanzania (TTB), imesitisha leseni zote za biashara za makampuni ya TLTC iliyokuwa yananunua zao hilo, baada ya kukaidi maagizo ya Serikali yaliyoitaka kuwalipa wakulima fedha wanazodaiwa kama malipo ya pili.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikoa cha bodi mwishoni mwa wiki mjini Tabora chini ya Mwenyekiti wake, Vita Kawawa, ambaye alisema kampuni hiyo ilikaidi kufanya malipo hayo kama ilivyoagizwa.
Kawawa alisema kutokana na maelekezo hayo, leseni za biashara za kampuni hiyo zinasitishwa hadi pale itakapowalipa wakulima malipo yao ya pili na kuwataka viongozi kusimamia utekelezaji huo.
Alisema wajumbe wa bodi yake walitembelea wilaya za Uyui, Sikonge, Urambo na Kaliua kwa lengo la kuona changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa zao la tumbaku na kukutana, ambapo walibaini masuala kadhaa ikiwamo malalamiko ya wakulima kutolipwa fedha zao.
Akizungumzia upatikanji wa pembejeo, Kawawa alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, imebadili utaratibu wa upatikanaji pembejeo na kufanikiwa kuishusha kutoka Dola 52.3 kwa mfuko wa NPK msimu uliopita hadi dola 40.45
Alisema wameweka utaratibu wa wazalishaji kuzifikisha pembejeo hizo moja kwa moja kwenye chama cha msingi pasipo kupitia tena kwa wauzaji wa kati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Wilfred Mushi, alisema wadau wa tumbaku wanapaswa kuhakikisha wanafuata sheria ili kudumu katika sekta hiyo.
Alisema sheria haitabagua na itamkumba yeyote katika sekta ya tumbaku atakayevunja sheria wakiwamo wakulima wenyewe.