KINSHASA, Congo DRC
UKIWA umebaki muda usiozidi mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu uliosubiriwa kwa muda mrefu nchini hapa, kiongozi mkuu wa upinzani, Felix Tshisekedi anatarajiwa kurejea mjini kuzindua kampeni zake akigombea nafasi ya urais.
Felix Tshisekedi ni mtoto wa Etienne Tshisekedi, aliyefariki dunia mwaka jana baada ya kutumikia miongo kadhaa katika kambi ya upinzani nchini.
Felix ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais na mwenzake, Vital Kamerhe kama mgombea mwenza.
Habari zilizopatikana mjini hapa zinaeleza kwamba Feilix na Kamerhe, wa chama cha UNC, wanatarajiwa kuzindua kampeni zao kwa pamoja, baada ya makubaliano ya kuunganisha nguvu hali ambayo wengi wanaitazama kuwa italeta mgawanyiko wa kura za wapinzania katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miezi minne tangu vyama vya upinzani vikubaliane kusimamisha mgombea mmoja ambako Mbunge aliyekuwa hajulikani na wengi, Martin Fayulu, aliteuliwa kugombea nafasi ya urais kwa niaba ya muungano wa vyama vyote.
Hata hivyo muda mfupi baada ya makubaliano hayo, vyama vya UDPS na UNC vilijitoa kwenye muungano huo.
Tshisekedi sasa atawania nafasi ya urais kwa makubaliano kwamba Kamerhe atakuwa waziri mkuu wake .
Mpaka sasa ni wagombea 19 wanaowania nafasi moja ya urais akiwamo mgombea wa chama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary.
Taarifa zilizopo nchini hapa na za kutoka kwa mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mbelechi Msochi, zinasema vyama vya upinzani vinalalamika kutokuwa na fedha za kuendesha kampeni zao.
Kwa sababu hiyo vinajibana na fedha ndogo vilivyo nayo mpaka wiki mbili kabla ya uchaguzi ndipo vitakapoingia mchuano wa kunadi sera zao kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.
Uchaguzi huo ambao umecheleweshwa kwa miaka miwili sasa unatarajiwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu.