BILIONEA Donald Trump amemwagia sifa Rais wa Urusi, Vladimir Putin wakati wakijibu maswali ya wanajeshi wastaafu pamoja na mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais, Hillary Clinton.
Mgombea huyo wa Chama cha Republican alisema Putin ‘amekuwa kiongozi kwa kiwango kikubwa kumshinda rais wetu (Obama)’.
Alisema hayo siku ambayo Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeituhumu Urusi kupanda mbegu za uhasama na misukosuko duniani.
Hillary kwa upande wake ametetea uwezo wake wa kufanya maamuzi ya busara, huku akiendelea kushutumiwa kutokana na sakata ya barua pepe.
Anadaiwa kutumia anuani binafsi kutuma na kupokea nyaraka rasmi za Serikali, jambo ambalo baadhi wanasema huenda lilihatarisha usalama wa taifa.
Trump aliulizwa maswali na mtangazaji wa NBC, Matt Lauer kuhusu matamshi yake ya awali akimsifu Putin.
Alijibu: “Ninaweza kumpa asilimia 82 kwa uongozi mahiri. Nafikiri anaponisifu, nitazikubali pongezi hizo. Putin amelidhibiti vyema taifa lake na wananchi wake wanampenda kwa asilimia 82.”
Trump pia alibashiri kwamba akichaguliwa kuwa Rais Novemba mwaka huu ataelewana vyema na Putin.
Hii si mara ya kwanza kwa Trump kumsifu kiongozi huyo wa Urusi. Desemba mwaka jana, alisema ilikuwa ni ‘heshima kubwa’ pale Putin alipomweleza kama ‘mtu mwenye kipaji’.
Hivi karibuni, Trump alishutumiwa alipohimiza Urusi kufukua zaidi kuzipata barua pepe ambazo Hillary alizifuta kutoka kwenye faili la kutunzia, ambazo inaaminika zilipotea.
Baadaye alijitetea na kusema alikuwa anatania.