WASHINGTON, MAREKANI
MTANDAO mmoja wa habari mjini hapa umeripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amewaeleza wasiri wake kuwa ataiondoa Marekani kutoka mkataba kuhusu makubaliano ya kihistoria ya tabia nchi.
Kutokuwepo kwa uhakika juu ya msimamo wa Marekani kuhusu mkataba huo wa Paris kuliwaghadhabisha baadhi ya wakuu wa nchi waliohudhuria mkutano wa kilele wa mataifa yaliyostawi kiviwanda (G7) uliomalizika juzi nchini Italia.
Mtandao huo umetumia vyanzo vitatu vilivyo na uelewa kuhusu mipango ya Trump.
Aidha umeangazia Shirika la Habari la Axios, linaloheshimika nchini Marekani, ambalo limeripoti juzi kuwa Rais Trump aliwaambia msimamo wake huo washauri wake wakuu wa karibu.
Mkataba huo wa Paris unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabia ulifikiwa mwaka 2015, lakini umekuwa ukisuasua kutokana na Marekani kuhofia utaua viwanda vyake.
Axios limemtaja mkuu wa wakala wa ulinzi wa mazingira nchini Marekani Scott Pruitt, kama miongoni mwa watu wachache waliopewa taarifa za mpango huo.