OHIO, MAREKANI
MGOMBEA urais wa Chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump ametangaza sera zake kuhusu usalama wa taifa, akiapa kuufanyia mageuzi mchakato wa uhamiaji ili kuwazuia wale aliowataja wasiozingatia maadili ya Marekani.
Katika hotuba yake aliyoitoa juzi jimboni hapa, Trump alizungumzia masuala kadhaa yakiwemo hatua za kiusalama atakazochukua iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Lengo la hatua hizo pamoja na mambo mengine alisema ni kuwaangamiza wanamgambo wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) na kukabiliana na ugaidi.
Kwa sababu hiyo, alisema atahakikisha wahamiaji wanafanyiwa uchunguzi wa kina kabla ya kuruhusiwa kuwa sehemu ya taifa hili na kuwazuia wanaotoka nchi hatari kuleta ugaidi.
Mbali ya hayo alisema kutakuwepo mifumo ya uchunguzi ikiwa ni pamoja akaunti zao za mitandao ya kijamii.
Aidha alisema akichaguliwa kuwa rais Novemba 8 mwaka huu, atabadilisha sera za mambo ya nje za nchi hiyo kwa lengo la kujenga taifa kwa kuwa na sera zenye uhalisia.
Aidha Trump amesema yuko tayari kufanya kazi na nchi yoyote ile bila kujali tofauti za kiitikadi au mikakati akiwa na nia ya kusaidia kulitokomeza IS.