WASHINGTON, MAREKANI
MCHUNGAJI wa Kimarekani aliyeachiliwa huru baada ya kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani nchini Uturuki kwa miaka miwili, jana alikutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika Ikulu ya White House.
Kuachiliwa huru kwa Andrew Brunson, kunaangaliwa kama ushindi wa kidiplomasia kwa Trump ambaye anatarajia kuungwa mkono na Wakristo wa makanisa ya Kiinjili kwa wagombea wake wa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika mwezi Novemba.
Mahakama ya Uturuki juzi ilimhukumu mchungaji huyo kifungo cha miaka mitatu jela kwa mashtaka ya kuhusika na shughuli za kigaidi. Lakini mchungaji huyo wa Kiinjili mwenye umri wa miaka 50, aliachiliwa huru kwa vile tayari alikuwa ameshawekwa kizuizini kwa miaka miwili. Mashtaka ya awali yaliyokuwa yakimkabili yanayohusu ujasusi pia yamefutwa.