Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
TRENI ya abiria ya Deluxe iliyokuwa safarini kutoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam, imepata ajali katika Stesheni za Ngeta na Ruvu mkoani Pwani.
Ajali hiyo ilitokea jana jioni baada ya kuacha njia na kusababisha mabehewa kuanguka.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez, alisema ajali hiyo ilihusisha mabehewa matano na kati ya hayo manne yalikuwa ya abiria na moja ni lile la breki linalokaa nyuma.
Alisema mabehewa mawili yaliacha njia na matatu yalianguka.
“Hiyo treni ilikuwa inatokea mkoani Kigoma na ilitakiwa kufika Dar es Salaam saa 11:30 jioni, lakini muda huu (saa 10:39 jioni) tumepata taarifa kwamba imepata ajali, bado tunaendelea kufuatilia kujua kama kuna majeruhi,” alisema Maez.
Alisema tayari wahandisi na mafundi wa TRL wameelekea katika eneo ilikotokea ajali hiyo.
Alisema ilitokea saa 9:40 alasiri ambapo wapo kadhaa wamejeruhiwa na mmoja hali ni mbaya.
“Kikosi cha uokoaji kikimaliza kazi ya kuinua mabehewa ndipo taarifa za waathirika itatolewa kwa umma,” alisema.