Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Uhakika na usalama wa mizigo inayopitia Zanzibar sasa utaongezeka baada ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuingia makubaliano na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 5,2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Mwenda, wakati wa kusaini makubaliano na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) kurahisisha shughuli za biashara zinazotumia forodha Zanzibar.
Amesema TRA ina jukumu la kikatiba la kusimamia kodi za forodha katika Jamhuri ya Muungano Tanzania hivyo watashirikiana kubadilishana taarifa mbalimbali kwa kutumia mifumo kabla ya kuruhusu mizigo itoke kwenye bandari za Zanzibar.
Aidha amesema kabla ya kuingia makubaliano hayo mizigo ilikuwa inachukua muda mrefu lakini sasa utapungua na kuondoa vikwazo na urasimu uliokuwepo awali.
Kamishna huyo amesema mwelekeo wao ni kuwa na makubaliano na taasisi kaguzi 13 ili kurahisisha utoaji wa mizigo Zanzibar na shughuli za biashara.
Naye Mkurugenzi wa ZBS, Yusuph Majid Nassoro, amesisitiza kuwa hawataruhusu bidhaa yoyote kuingia visiwani humo kama mtu hana Namba ya Mlipakodi (TIN) ili waweze kutambulika na kulipa kodi za Serikali.