Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
Kampala ya Mapato Tanzania (TRA), leo imekutana na jumuiya ya wafanyabiashara wa china ili kuwapa elimu ya kodi itakayowawezesha kufanya biashara zao bila usumbufu.
Akizungumza baada ya semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Tanzania (BOT), Meneja Msaidizi wa Madeni na Ulipaji Kodi kwa Hiyari Kariakoo kutoka TRA, Daudi Deokari amesema wafanyabiashara wa China ni wawekezaji wakubwa nchini na kwamba wamekuwa wakikutana na changamoto ya kutokujua lugha pamoja na sheria za nchi.
Amesema katika mafunzo hayo wamefundishwa sheria za kodi pamoja na taratibu wanazotakiwa kufuata zitakazowawezesha kufanya biashara bila usumbufu.
“TRA imekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mbalimbali ili kuwapa elimu ya kodi hasa ikizingatiwa kuwa sheria zimekuwa zikibadilika kila mwaka,” amesema Deokari.
Amesema wafanyabiashara wa China wamekuwa na changamoto ya lugha ikiwa ni pamoja kukutana washauri wa kodi ambao si sahihi na kuwapotosha na kwamba utaratibu wa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara ambao ni wawekezaji ni endelevu kwa nchi nzima.