25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TRA yatua kwa Chenge, Tibaijuka

1MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetua kwa vigogo waliopata mgawo wa fedha za Escrow na kuwataka kulipa kodi ya mapato kwa mujibu wa sheria.
Maofisa wa mamlaka hiyo walikwenda kwa vigogo hao na kuwasilisha mahesabu ya kodi walizochukua Januari Mosi mwaka huu ambapo kila aliyepata mgawo huo ametakiwa kulipa fedha hizo kabla ya Januari 30.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema msimamo wa Serikali unabaki kama ulivyo wa kuhakikisha kila mmoja analipa kodi ya mapato kwa mujibu wa sheria.
Mwigulu alisema baada ya wahusika hao waliopata mgawo huo wa fedha za Escrow kupelekewa hesabu za kodi, wametakiwa kuhakikisha wanahakiki ndani ya mwezi mmoja na kodi iwe imelipwa.
Waliopelekewa hesabu za kodi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) na aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka waliopata mgawo wa Sh bilioni 1.6 kila mmoja, ambao wanatakiwa kulipa kodi Sh milioni 480 kila mmoja.
Wengine ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, Jaji Aloysius Mujulizi pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko ambao kila mmoja alipokea Sh milioni 40.4. Hao kila mmoja anatakiwa kulipa kodi ya Sh milioni 12.12.
Wengine ni aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku aliyepokea Sh milioni 161.7, ambaye anatakiwa kulipa kodi Sh milioni 48.5 na Profesa Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.25) akitakiwa kulipa kodi Sh milioni 121.27.
Pia wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko aliyepata mgawo wa Sh milioni 40.4 (kodi Sh milioni 12.12 ), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo Sh milioni 80.8 (kodi Sh milioni 24.24) na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini Sh milioni 80.9 (kodi Sh milioni 24.27).
Kutokana na hesabu hizo kila aliyepokea fedha hizo anatakiwa kulipa asilimia 30 ya kodi ya mapato.
Kwa mujibu wa mgawo huo wa fedha za Escrow uliotolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering Ltd, James Rugemalira, jumla ya kodi iliyotaka kukwepwa na vigogo hao ni Sh bilioni 1.275.
Naibu Waziri Mwigulu alisema wamelazimika kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato (Income Tax Act) ya 2012 ambayo inaelekeza mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za mapato yake kwa TRA kila ifikapo mwisho wa mwaka ambazo huiwezesha mamlaka hiyo kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.
Mwigulu ambaye jana alikuwa katika sherehe ya kutimiza umri wa miaka 40 ya kuzaliwa kwake, pamoja na mambo mengine alifanya shughuli za kijamii ikiwamo ziara kwenye Hospitali ya Mwananyamala, kituo cha kulelea watoto yatima na kituo cha kutolea damu salama cha Msimbazi Center. Pia alifanya mazungumzo yaliyochukua saa moja katika kituo cha redio cha Clouds FM.
Katika mazungumzo yake hayo aligusia mambo mbalimbali muhimu ya kiuchumi ikiwamo suala la ukwepaji wa kodi, sakata la uingizaji sukari ya magendo na misaada ya wahisani.
Alisema kuna haja ya kurekebisha sheria ili kuwabana wabadhilifu wa fedha za umma ambao licha ya kuachia nyadhifa za Serikali wanapaswa wafilisiwe mali pamoja na kuchuliwa hatua za kisheria.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema ubadhilifu ukitokea lazima anayehusika atiwe nguvuni kwa ajili ya kupisha vikwazo katika kuendesha kesi.
“Anayesababisha upotevu au kuiba Sh bilioni 30, akiachwa nje atahonga, ndiyo maana kila siku tunasikia Serikali imeshindwa katika kesi kama vile mawakili wetu ni wa darasa la saba na wale watetezi wa wezi ni maprofesa,” alisema.
Alisema enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuwa mkali kwa watuhumiwa wa rushwa na alikuwa haruhusu hakimu aamue suala ambalo lilikuwa limewekwa kwenye sheria.
Mwigulu alisema wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere sheria ilikuwa inataka mtu anayethibitika amekula rushwa achapwe viboko 12 anapoingia jela na akitoka 12 ili akamuonyeshe mke wake nyumbani.
“Sasa mtu amechukua Sh bilioni 8 alafu unakwenda kumshtaki na anayeendesha mashtaka ana posho ya Sh 80,000 hili ni tatizo, nasubiri tutakapokuwa tunarekebisha sheria tukubaliane kwenye mambo ya kodi tuwe wakali na wale wanaokwepa kodi na kwa watumia vibaya kodi,” alisema Mwigulu.
Alisema suala la ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya mali za umma linaweza kufikia kikomo endapo wahusika watatangazwa na kupewa adhabu kali mbali na kuwafukuza kazi au kurudisha kodi walizokwepa.

KASHFA YA SUKARI
Akizungumzia kuhusu kashfa ya uagizaji haramu wa sukari iliyotikisa hivi karibuni, Mwigulu alisema wiki mbili zilizopita kuna kikao kilikaa cha wadau wa sukari na Wizara ya Kilimo na Chakula na kukubaliana kuhusu wafanyabiashara kununua sukari za viwandani.
Alisema suala hilo haliondoi wajibu wa mambo mawili, ikiwamo ukweli wa viwanda vilivyopo nchini pamoja na kuzalisha lakini kuna upungufu unajitokeza wa tani 1,50,000.
Mwigulu alisema hali hiyo pia haiondoi ukweli kwamba Serikali ilishafuta utaratibu wa vibali vya kuingiza sukari na vitu kama mchele na vinginevyo bila kulipiwa ushuru.
Alisema Serikali kupitia vyombo vinavyohusika itaendelea kusimamia na kuhakikisha inazuia sukari zinazoingia kwa njia za ‘panya’ ambazo zinakuwa hazijalipiwa kodi wala kufuata utaratibu na viwango vya ubora.
Aliongeza pia kutakuwa na miundombinu na utaratibu kuhakikisha sukari inayoingia ina kumbukumbu ili kuangalia kiwango ambacho kitakidhi mahitaji yaliyobaki kwa lengo la kuhakikisha viwanda vya ndani havikosi soko.

MISAADA YA WAHISANI
Akizungumzia msimamo wa wahisani kuzuia misaada kwa Tanzania, Mwigulu alisema Serikali imelazimika kutumia fedha za ndani kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya kupeleka katika shughuli za maendeleo.
“Katika nusu mwaka huu wa kwanza tumetoa zaidi ya Shilingi bilioni 200 kwenda kwenye miradi ya maendeleo katika maeneo ya maji, umeme vijijini, mikopo ya elimu ya juu,” alisema.
Alikiri kwamba suala la wafadhili kukataa kutoa misaada lilikuwapo, lakini waliridhika na ripoti iliyosomwa na sasa wameshatoa kama watatu na wengine walikuwa tayari wameshatoa.
Akizungumzia kuhusu asilimia 40 ya bajeti kutegemea fedha za wahisani, alisema lilipotokea suala la kusuasia misaada ilisababisha kuchelewa kwa fedha za maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles