28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu: auchungulia urais

SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
KASI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, imezidi kuongezeka baada ya Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kuonyesha nia ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alionyesha nia hiyo huku akitumia nukuu za mitume, akiwamo Yesu Kristo kupitia kitabu kitakatifu cha Biblia.
Mwigulu alionyesha nia hiyo jana, akiwa katika maadhimisho ya kutimiza miaka 40 ya kuzaliwa kwake.
Awali asubuhi ya jana, alianza kwa kualikwa katika kipindi maalumu na kituo cha Radio Clouds FM cha jijini Dar es Salaam ambacho kilirushwa kwa muda wa saa moja.
Pamoja na mambo mengine, Mwigulu alizungumza masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwamo matumizi ya rasilimali za taifa na viongozi wake.
Baada ya kumaliza kipindi hicho, aliambatana na wasaidizi wake wakiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) kabla ya kuhamia CCM, Juliana Shonza na Mwisho Mwampamba hadi Hospitali ya Mwananyamala, ambako alitembelea wagonjwa na kuchangia damu kwa ajili ya wajawazito.
Akizungumza na waandishi wa habari ambao walimuuliza kuhusu kugombea urais mwaka huu, Mwigulu alisema swali hilo amekuwa akiulizwa kila mara na makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi wa elimu ya juu, wakulima, wafugaji na Watanzania wanaoishi nje ya nchi, lakini amekuwa akisita kufanya hivyo kutokana na nafasi yake ndani ya chama.
“Hata nilipokuwa kwenye moja ya mkutano wangu mkubwa wa mjini Geita, wananchi walinipatia ujumbe uliokuwa umeandikwa katika bango wakiuliza kama mimi ndiye kiongozi kutoka Kanda ya Ziwa nitakayewania urais au wamsubiri mwingine,” alisema.
Hata hivyo, akitumia maneno ya kwenye Biblia kujibu swali hilo, alisema wakati wa zamani Yesu alivyowapata wanafunzi wa Yohana mbatizaji walitaka kujua kama ndiye Yesu aliyetangazwa na Yohana kwamba atakuja.
“Yesu aliwaambia wanafunzi wale wa Yohana waende wakamwambie kwamba vipofu wataona, viwete watatembea, wagonjwa watapona, viziwi watasikia… pia mkamwambie kuwa heri wasio na mashaka nami,” alisema Mwigulu.
Lakini pamoja na kusema hayo, Mwigulu alisema suala la urais kulitoa moja kwa moja kutokana na nafasi yake ndani ya chama na ndani ya Serikali analivutia pumzi.
“Kwa sasa nimejikita zaidi kutimiza wajibu wangu kumsaidia Waziri wa Fedha ili masuala ya uchumi yakae sawa na katika chama changu, sitaki kuonekana kama mmoja wa wavunjifu wa maadili kwa sababu nahusika na usimamizi wa maadili, hivyo sitaki kuyavunja,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu baadhi ya makada waliotangaza kujitokeza hali ya kuwa wapo ndani ya Serikali, Mwigulu alisema suala la cheo cha mtu serikalini si kigezo cha kuwa rais ila linatokana na utendaji wa mtu.
“Watanzania sasa wana uwezo wa kujua na kuchambua kila kitu, mtu kuwa serikalini si kigezo cha kumfanya kuwa rais ila ni utendaji, hata marehemu Edward Sokoine alipokuwa akipendwa wakati huo si kwa sababu ya cheo chake ila utendaji wake,” alisema Mwigulu.
Kujitosa kiaina katika kinyang’anyiro cha urais kwa mwanasiasa huyu kunaongeza idadi ya makada wa CCM ambao wamekuwa wakitajwa katika mbio hizo wakiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Taknolojia January Makamba.
Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu, Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah, na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles