23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC Nyamagana awatoa hofu wananchi usalama wa chanjo ya corona

Na Clara Matimo, Mwanza

Kufuatia uwepo wa sintofahamu inayoleta hofu kwa wananchi juu ya uchanjaji wa chanjo ya Covid -19 inayotarajiwa kuanza kutolewa  karibuni kwa makundi maalum, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, Amina Makilagi, amewatoa wasiwasi wananchi juu ya usalama wa huduma hiyo na kuwataka kuiamini Serikali.

Amina ametoa wito huo Julai 27, jijini hapa alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuhudhuria kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe, Chanjo ya corona, Huduma za kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na Huduma ya afya ya Mama na Mtoto kilichoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Mwanza.

 “Watanzania wenzangu nawaomba wapuuze maneno ya baadhi ya watu wanayoyatoa kuhusu athari za chanjo hiyo kwanza watambue kwamba chanjo zote tunazochanjwa Tanzania ziwe za watoto au za mama wajawazito zinatoka nje ya nchi hakuna chanjo inayotengenezwa hapa nchini   kwa hiyo mimi nawaambia wananchi wasiwe na wasiwasi wawapuuze hao wanaowatisha.

Amesema serikali haiwezi kufanya jambo baya kwa wananchi wake wala kuwapa chanjo ambayo itawaletea madhara kwani wajibu wake ni kuwalinda raia wake.

“Mataifa yaliyotengeneza  chanjo ya Covid-19 yamekuwa yakishirikiana na nchi yetu muda mrefu katika chanjo mbalimbali pamoja na kutugawia bure vidonge vya ARV ambavyo vinawasaidia wanaoishi na maambukizi ya VVU, hivyo wangekuwa na dhamira mbaya ya kutuuwa wengi tungeishakufa maana chanjo zao nyingi tumeishachanjwa, mimi ninaongea nikiwa na ushahidi maana nimehudumu katika kamati ya masuala ya ukimwi,”amesema na kuongeza

“Mimi binafsi nitakuwa mtu wa kwanza  kuchanjwa katika Wilaya ya Nyamagana kwa kuwa nimeelezwa faida zake nimeridhika na ninajua Rais wetu Samia Suluhu Hassan, anania ya kutulinda wananchi wake ili tusipate maambukizi ya ugonjwa wa corona ndiyo maana ametuletea chanjo hii tena kwa hiari sio lazima hivyo ni wajibu wetu kuiamini Serikali yetu na viongozi wake,”amesisitiza.

Amewataka wananchi kutambua kwamba watakapo chanjwa watakuwa wamejikinga pia hawatapata maambukizi ya ugonjwa huo  kwa sababu watakuwa na kinga ambayo itawasaidia kuwaweka salama zaidi.

“Naamini baada ya sisi wananchi wa awamu ya kwanza kupata chanjo, kadri tutakavyoendelea watanzania wenzetu wakiona matokeo ambayo kwa hakika yatakuwa ni mazuri  nao  watakuja kuchanjwa bila wasiwasi kwa sababu watakuwa wameishaona mafanikio kwa sisi tuliotangulia,” amesema.  

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema  maandalizi ya kutoa chanjo mpya ya Covid-19 yanaendelea vizuri na wameisha ainisha  vituo vya  kupambana na corona kwa njia ya chanjo huku naye akiahidi kuwa wa kwanza kuzindua chanjo hiyo mkoani humo kwa kuchanjwa.

“Mimi natambua faida za chanjo hiyo hivyo nitakuwa wa kwanza kuchanjwa nawaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza wajitokeze kwa wingi baada ya uzinduzi ili nao wachanjwe waweze kujikinga na maambukizi wasiwasikilize watu wasio na utaalamu wa masuala ya afya.

“Sasa hivi kila mtu ni mtaalamu wa masuala ya afya kumekuwa na siasa nyingi mno chafu  kila mtu anazungumza kama ni mtaalamu wa masuala ya afya sielewi lengo lao ni nini hao ndiyo wenye nia ya kuwapotosha watanzania ili waangamie lakini viongozi wa Serikali tutaendelea kuwapa elimu  watambue kwamba chanjo ni salama kabisa na nia ya Serikali ni kuwalinda,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles