26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Likizo ya corona yaacha wanafunzi 12 na mimba Njombe

Na Elizabeth Kilindi-Njombe

WANAFUNZI 22 wa shule za sekondari mkoani Njombe wamepata mimba wakati wa likizo ya corona Machi hadi Aprili mwaka huu, huku moja ya sababu ikitajwa ni pamoja na wazazi, walezi kutokuwa karibu na watoto wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issa, aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa hivi karibuni ofisini kwake.

Kamanda Issa alisema mimba hizo ni kwa kipindi cha Machi hadi Aprili, hivyo kuwataka wazazi na walezi kutimiza jukumu la malezi kwa watoto hao kuwaepusha na changamoto hiyo.

“Jukumu la malezi linapaswa kuzingatiwa ili waweze kuwa salama, tuwasaidie watoto hawa ili wasikutane na hao vijana wanaowawinda, nisisitize kipindi cha likizo wazazi walezi angalieni watoto,” alisema Kamanda Issa.

Alisema Jeshi la Polisi limeweka mikakati mbalimbali, ikiwemo kushughulikia kesi zote za mimba mashuleni na kwamba wote waliohusika hawatoachwa.

“Hatutawaacha wanaosababisha mimba kwa wanafunzi na tayari baadhi ya watuhumiwa walifikishwa mahakamani na kufungwa vifungo,” alisema Kamanda Issa na kuongeza kuwa wahanga wamekuwa wakitoa taarifa mapema kituoni kutokana na elimu wanayopata.

Pia alisema Jeshi la Polisi linaendelea na mikakati yake ya kupambana katika kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii ili kuweza kupunguza tatizo la mimba mashuleni.

Jonson Mgimba, mkazi wa mjini Njombe, alisema adhabu inayotolewa kwa wanaowapa mimba wanafunzi haitoshi ndio maana vitendo hivyo vimeendelea kushamiri.

“Adhabu ziongezwe kwa hawa wanaosababisha haya ili kukomesha, adhabu kubwa inahitajika, mtoto wa kike anakabiliwa na adhabu kubwa ya kukosa masomo na hilo lipo kichwani kwake,” alisema Mgimba.

Pia alisema bado jamii inakabiliwa na tatizo kubwa la kuporomoka kimaadili kuanzia ngazi ya familia.

“Utandawazi Tanzania tumeupokea vibaya ambao umesababisha kuporomoka kimaadili. Kumeathiri wazazi, kumeathiri watoto wenyewe, kuna familia zinakuwa karibu na mtoto, lakini nyingine wala hazijali kuhusu mtoto, hivyo wanashindwa kujilea wenyewe,” alisema Mgimba.

Alisema pia shughuli za kujitafutia kipato kwa wazazi na walezi zimekuwa zikiwaacha huru watoto, hivyo kusababisha kupata majanga mbalimbali, ikiwemo ubakaji na mimba za utotoni.

“Tunapowaacha watoto peke yake muda mwingi wanashinda katika kuangalia luninga na simu, na hali ya uchumi ilivyo kwa sasa wazazi tuko bize katika utafutaji wa hela mpaka tunasahau familia zetu,” alisema Mgimba. 

Agnes Mdeme, mkazi wa mjini Makambako, alisema kujisahau kwa baadhi ya wazazi na walezi katika malezi kunachangia kuharibu ndoto za mtoto wa kike.

“Mtoto wa kike anapopata mimba haruhusiwi kurudi shule, hii ni adhabu kubwa kwake, niwasihi wazazi wenzangu tubadilike, tuwe karibu na watoto wetu ili kuwalinda na watu wabaya,” alisema Agnes.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles