NA Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA) imekusanya kodi ya sh trilioni 10.87 katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka wa fedha 2016/17 kuanzia Juni 2016 hadi Machi 2017.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, ilieleza kwamba makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa makusanyo kwa asilimia 9.99 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2015/16 ambapo makusanyo yalikuwa asilimia 9.88.
Alisema katika mwezi wa Machi 2017,TRA imekusanya Sh trilioni 1.34 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.31 ya Machi 2016 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 2.23.
Alisema, TRA inawashukuru walipakodi wote ambao wameitikia wito wa kulipa kodi ya Serikali kwa hiari na hivyo kuiwezesha mamlaka hiyo kutimiza wajibu wake kwa kisheria.
Alisema , TRA inatoa wito kwa kila mlipakodi kuwajibika kulipa kwa wakati pamoja na kufichua wale wasiotimiza wajibu wao kikamilifu ili Serikali iweze kutimiza malengo waliyokusudia kwa wananchi wake.
“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, mamlaka kwa kipindi cha mwaka wa fedha kilichobaki cha miezi mitatu kinachoanza Aprili mpaka Juni itaelekeza kujudi zake katika kukusanya kodi mbalimbali.
“Kuhakikisha kuwa lengo la mwaka la kukusanya kodi shilingi trilioni 15.1 inafanikiwa, hivyo TRA itaendelea na mpango wake wa kukusanya kodi za majengo kwa kutoa viwango maalumu vya kodi kwa majengo mikoa mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa wadau,” alisema Kayombo
Kutokana na hali hiyo aliwataka wamiliki wa majengo ambayo bado hayajafanyiwa tathmini wanajulishwa kufika kwenye ofisi za TRA za mikoani au kutembelea tovuti ya mamlaka hiyo kwa ajili ya kuangalia viwango vya kodi.
Alisema, TRA wanazidi kusisitiza kuwa, matumizi ya mashine za EFD pamoja na zoezi la uhakiki wa TIN katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza,Mbeya,Dodoma, Morogoro,Tanga na Pwani linaendelea, hivyo wananchi wanaombwa kuhakikisha wanatumia EFD na wale wa mikoa husika wanahakiki TIN zao ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.