23.6 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaanza kampeni ya kuhamasisha matumizi ya EFD

Na Mwaandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wanunuzi kudai na kukagua risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.

Akizungumza leo Desemba 7, 2021 wakati wa kampeni hiyo iliyoanza katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Msimamizi wa Kitengo cha EFD wa Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Hamidu Shaban alisema kuwa, zoezi hilo ni endelevu na linafanyika katika maeneo yote ya Dar es Salaam.

“Tunafanya zoezi hili katika mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti kuanzia kwenye mizigo yote inayozalishwa viwandani na kupelekwa madukani inauzwa kwa risiti na kuhakikisha wale wanaonunua bidhaa wanadai risiti,” alisema Shaban.

Shaban amezitaja adhabu za kutokutoa na kudai risiti kuwa ni shilingi milioni 1,500,000 hadi 4,500,000 kwa wafanyabiashara wasiotoa risiti za EFD na wanunuzi wasiodai risiti, adhabu ni Sh 30,000 hadi Sh milioni 1,500,000.

Rehema Mbilinyi ni Mfanyabiashara wa Kariakoo ambaye amefurahishwa na zoezi hilo linalofanyika la kuhamasisha matumizi ya EFD ambapo ameiomba Serikali kugawa makundi ya wafanyabiashara wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuweka viwango tofauti tofauti vya VAT ili kuondoa tatizo la baadhi ya wafanyabiashara kutoa risiti pungufu au kutokutoa kabisa kwa kuogopa kuingia kwenye VAT.

“Kampeni hii ni nzuri lakini mimi naona kuna haja ya Serikali kutoza kodi ya VAT kwa kugawa makundi kwa mfano, wale wafanyabiashara wakubwa wawe na asilimia 18 kama kawaida, wafanyabiashara wa kati watozwe asilimia 10 na wasajiliwa wapya wa VAT waanze kwa asilimia 5. Hii itasaidia kupunguza tatizo la kutokutoa risiti au kutoa risiti pungufu,” alieleza Rehema.

Kwa upande wake, Sylivanus Nyigu ambaye pia ni mfanyabiashara wa Kariakoo, licha ya kuisifia kampeni hiyo, amesema zoezi hilo litasaidia kuondoa mapungufu yanayojitokeza kwenye suala zima la kutoa na kudai risiti na kuyatafutia ufumbuzi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania imekuwa na utaratibu wa kufanya kampeni za mara kwa mara kwa lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za EFD pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles