25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

TRA wakusanya Sh trilioni 3.8 kwa miezi mitatu

 

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh trilioni 3.84 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ikilinganishwa na Sh trilioni 3.65 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kiasi hicho ni sawa na ukuaji wa asilimia 5.32.

Alifafanua kuwa Julai walikusanya Sh trilioni 1.20, Agosti Sh trilioni 1.27 na Septemba Sh trilioni 1.36.

“Tunawashukuru walipakodi ambao wameendelea kulipa kodi zao kwa hiari na kwa wakati na tunawahimiza wale ambao bado wanasuasua kujitokeza kulipa,” alisema Kayombo.

Kuhusu misamaha ya riba na adhabu katika malimbikizo ya madeni ya nyuma, alisema hadi sasa wamepokea maombi 1,950 yenye thamani ya Sh bilioni 185.4.

Alisema baadhi ya waombaji wameshapewa majibu na mengine yako katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.

“Wafanyabiashara ambao hawajawasilisha maombi wawahi kabla ya Novemba 30 kwa sababu hatutegemei kuongeza muda,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema pia wamebaini kuwapo kwa udanganyifu katika matumizi ya mashine za EFD hasa maeneo ya Kariakoo na kuwaonya wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja.

“Wako wanaoghushi risiti za EFD na wengine unakuta wanatumia risiti moja kusafirishia mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, yaani siku nzima inatumika risiti moja tu,” alisema Kayombo.

Alisema pia kwenye vituo vya mafuta watu wengi wamekuwa hawachukui risiti na kutahadharisha kuwa kuna adhabu pande zote mbili yaani kwa mfanyabiashara na mteja.

Kwa mujibu wa Kayombo adhabu kwa mtu asiyetoa risiti ni faini kati ya Sh milioni 3 hadi 4.5, kufungwa au adhabu zote kwa pamoja na kwa asiyedai risiti adhabu ni faini kati ya Sh 30,000 na Sh milioni 1.5 kutegemeana na thamani ya bidhaa husika.

 

MAKONTENA YA MAKONDA

Katika hatua nyingine, Kayombo alisema makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, yatagawiwa bure.

Tayari minada minne ya kutafuta mnunuzi wa makontena hayo ilifanywa na Kampuni ya Udalali ya Yono, lakini hakuna mnunuzi aliyepatikana.

Alisema suala la makontena hayo linashughulikiwa kiutawala, lakini hakuwa tayari kutaja ni lini yatagawiwa na watu gani watanufaika.

“Taratibu zetu zinaturuhusu kunadi mara kadhaa tunavyoweza, lakini tunaweza kufanya uamuzi mwingine wa kugawa, sasa kugawa kwa nani hilo ni suala la utawala,” alisema Kayombo.

Sakata la makontena hayo lilianza Mei 12 mwaka huu, baada ya TRA kutoa notisi ya siku 30 kwa mizigo iliyokaa bandarini muda mrefu kukombolewa vinginevyo itanadiwa.

Hata baada ya kuisha kwa notisi hiyo, makontena hayo yalikuwa bado hayajaondolewa ndipo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliagiza yapigwe mnada huku akiapa kusimamia sheria na kanuni za kodi.

Makontena hayo yenye samani mbalimbali kama viti na meza, yalizuiwa kutolewa bandarini kutokana na kudaiwa kodi inayokadiriwa kuwa Sh bilioni 2.

 

MABASI YA UDART

Katika hatua nyingine, Kayombo alisema bado wanaendelea kuyashikilia mabasi ya Kampuni ya Udart kwa sababu wahusika hawajakamilisha taratibu za kodi za forodha ili yaweze kusajiliwa na kuingia barabarani.

Mabasi hayo 70 yaliyowasili tangu Februari mwaka huu, yamekwama katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kutolipiwa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles