UVCCM: Hamahama ya wapinzani ni demokrasia

0
758

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Hassan Bomboko, amesema hamahama ya wapinzani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni matokeo ya kuimarika kwa demokrasia.

Kuhusu madai ya baadhi ya watu wanaohoji gharama zinazotumika katika uchaguzi wa marudio ni maumivu kwa taifa, Bomboko alisema suala hilo hilo ni jukumu la wabunge kuamua kubadili sheria au laa.

Bomboko alitoa kauli hiyo jana alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya MTANZANIA, RAI, DIMBA na BINGWA.

Bomboko ambaye aliongozana na viongozi wengine wa idara hiyo alisema si kosa wala dhambi kwa watu kujiunga na vyama vingine vya siasa pale wanapoona ipo haja ya kufanya hivyo.

“Kuhama ni haki ya msingi na si kosa wala dhambi mtu kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine na wapo viongozi wa juu wa Chadema ambao walitoka CCM lakini waliaminiwa wakapewa ridhaa na sasa ni wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chao.

“Hoja hapa sasa ni namna gani tunadhibiti hizo fedha za walipakodi zisitumike kiholela, hili ni suala la wabunge kurudi bungeni wakiona kuna tija hiyo wafanye maamuzi kwa mamlaka yao mapana waliyonayo.

“Lakini mimi binafsi na vijana wa UVCCM tunaunga mkono hoja ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wanaoona ndani ya vyama vyao hakuna utulivu waje kwetu tutawapokea.

“Na sisi kupitia Ibara ya 8 ya Kanuni ya UVCCM jukumu letu kubwa ni kupokea maelekezo ya kutoka ngazi ya juu, vikao vya Kamati Kuu vimeamini kuwa hawa watu wanayo nafasi ya kupokelewa sisi tunawapokea.

“Niwaombe tu wenzangu tujaribu kuangalia wapi tulipojikwaa kama vyama vya kisiasa, tupitie zile hoja za wanaoondoka, tusiwabeze tutazame utashi wao kisiasa uko wapi, turejee katika misingi ya kiitikadi na kisera,”alisema Bomboko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here