29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

TRA na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha yateketeza mashine 16

KOKU DAVID, RUKWA

Mamlaka ya Mapato Mkoani Rukwa (TRA) kwa kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania imekamata na kuziteketeza mashine 16 za mchezo huo ambazo zilikuwa zimewekwa katika maeneo yasiyorasmi pia hazikuwa zimesajiliwa na bodi hiyo ikiwa ni pamoja na kutolipiwa kodi.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Kaimu Meneja wa TRA Rukwa, Chacha Gatora amesema kuwa wamekamata mashine hizo kutokana na ukiukwaji wa sheria uliofanywa na wamiliki na kwamba kwa mujibu wa sheria mashine hizo zinatakiwa kulipiwa kodi kila mwezi ikiwa ni pamoja na kusajiliwa katika bodi inayohusika na kusimamia mchezo huo.

Anasema mashine hizo zilizokamatwa ambazo ni mali ya kampuni tatu za Bonanza Ltd, JX Beting Ltd na Game Show zinamilikiwa na raia wa China.

Amesema uwepo wa mashine hizo mkoani Rukwa na nchini kwa ujumla ambazo hazifati sheria zinaukosesha mkoa  mapato pamoja na serikali.

“Niwahimize wafanyabishara mkoa wa Rukwa kuwa zoezi hili ni endelevu ili kuwabaini wale wote wasiofuata taratibu ikiwa ni pamoja na kutolipia kodi na lengo la mamlaka ni kuhakikisha watu wote wanaochezesha michezo hiyo wanachangia pato la serikali mkoani hapa kama sheria inavyoelekeza.

“Sehemu kubwa ya mashine hizi tulizokamata wafanyabishara hawa wamezipeleka  kuziweka katika maeneo ya vijijini ambako wanaona ni mbali maofisa wa TRA na jeshi la polisi hawawezi kufika pindi wanapofanya opareshini ya kuwakamata wakwepa kodi,” anasema Gatora.

Gatora anasema baada ya kuzikamata mashine hizo, hatua ya kwanza wamiliki walitozwa faini ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua ya kuziteketeza kwa moto ili iwe fundisho kwa wafanyabiashara wengine ambao sio wazalendo katika ulipaji kodi.

Anasema kwa mujibu wa sheria, kila mashine inatakiwa kulipa kodi ya shilingi 100,000 kila mwezi na kwamba ila kuepuka kuendelea kupoteza mapato ya serikali, TRA mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na bodi ya mchezo huo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi ili kuwawezesha kutambua mashine zilizosajiliwa na ambazo hazijasajiliwa.

Anaongeza kuwa mashine zilizosajiliwa ni zile zilizobandikwa stika ya bodi ya kusimamia mchezo huo na kwamba zile ambazo zitakuwa hazijabandikwa haziruhusiwi kutumika.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Mchezo wa Kubahatisha Tanzania, James Mbalwe anasema kuwa mchezo wa kubahatisha unachangia upatikanaji wa mapato ya nchi na kwamba katika mwaka wa fedha uliopita kiasi cha  shilingi bilioni 95 zilipatikana kutokana na mchezo huo.

 Amesema mchezo wa kubahatisha unaruhusiwa kisheria kwa mujibu wa sheria ya michezo ya kubahatisha ya mwaka 2003 na kwamba mashine hizo zilizokamatwa zilikuwa ni feki huku nyingine zikiingizwa nchini kinyume cha sheria.

Amesema mashine hizo zina thamani isiyozidi milioni 30 na zilikuwa zimewekwa katika maeneo yasiyokubalika kisheria.

“Sisi kama bodi tunajukumu la kuhakikisha kwamba michezo hiyo inaendeshwa katika maeneo yanayokubalika kisheria na watoto chini ya miaka 18 hawaruhusiwi watakaobainika kuwachezesha watachukuliwa hatua.

“Pia kwa wale watakaoendesha michezo hiyo katika maeneo yaliyosajiliwa na bodi naomba waruhusiwe kutokana na kuwa ni wafanyabiashara kama ilivyo wafanyabiashara wengine,” amesema Mbalwe.

Mbalwe anasema kuwa bodi ya mchezo huo itaendelela kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa mchezo huo na kwamba mashine za mchezo huo zinatakiwa kuwa katika maeneo yenye baa na maduka maalumu na si vinginevyo.

Anaongeza kuwa bodi inatoa stika kwa kila mashine iliyosajiliwa na kwamba kwa mashine isiyokuwa na stika ni batili.

Anasema kutokana na udogo wa taasisi ofisi zipo Dar es Salaam na Dodoma lakini wanatarajia kufungua ofisi nchi nzima.

“Asilimia 96 ya waendeshaji wa michezo hii wapo Dar es Salaam na mapato zaidi ya asilimia 90 yametoka huko ndo maana tupo karibu nao lakini kutokana na teknolojia tuna mradi wa tehama ambao utaturahisishia kuweza kuwafikia watanzania wote,” anasema Mbalwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles