27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ni upepo mpya au fursa CCM?

Na RATIFA BARANYIKWA-DAR ES-SALAAM

WIMBI la waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu limeleta taswira nyingine ya ndani ya chama hicho.

Hamasa ya sasa ya vijana,wanawake, wazee kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ndani ya CCM hata katika majimbo ambayo huko nyuma yaliogopwa na kuonekana kuwa ni ya akina fulani ni tofauti kabisa na ile ya mwaka 2015 na hapo kabla.

Watu wanaofuatilia mwenendo wa siasa nchini, watakubaliana nami kwamba kile kinachoonekana sasa kwa watu wengi tena wa kada tofauti tofauti kuchukua fomu ndani ya CCM hasa katika nafasi za ubunge na udiwani hakikuwahi kufika kwa kiwango cha sasa, miaka mitano, kumi au zaidi iliyopita.

Maprofesa, Madaktari, Waandishi wa Habari, Wanasheria, Watumishi wa Umma na watu wengine wa kada mbalimbali ni miongoni mwa waliojitokeza kwa wingi kuchukua fomu ndani ya CCM kiasi cha kila mmoja si tu kubaki na mshangao bali kujiuliza nini kilicho nyuma ya hamasa hii je ni upepo au kusaka fursa za kimaslahi?.

Profesa mbobevu wa sheria nchini, Issa Shivji kupitia ukurasa wake wa twitter, naye ameonekana kushangazwa na wimbi hilo  lakini yeye akigusa kada la taalama na  kwenda mbali akihoji sababu ya idadi kubwa ya  Maprofesa na Madaktari kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania ubunge.

Profesa Shivji amehoji je huko ni kukimbia taaluma? Au kusaka maslahi? madaraka? Fursa? kujilinda kisiasa? Uoga?

Maswali hayo ya Profesa Shivji yamejibiwa  kwa mtazamo tofauti na watu mbalimbali kupitia ukurasa wake huo huo wa Twitter,  mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Julius Nyang’ombe naye amemuhoji msomi huyo akiandika; 

“Kwani Bunge linatakiwa liwe la watu wa aina gani? kuwa Profesa isiwe sababu ya kutokuwa mbunge la sivyo tutaanza kubagua watu…kutunga sheria na kuisimamia Serikali yahitaji watu wenye utashi siyo kutimiza wajibu. Acheni watu wawe huru kwa kile wanachokiamini.

Richard Mabala katika hoja hiyo hiyo ameandika kwamba hatua hiyo  inazungumza kitu kuhusu mfumo wetu kwamba pale wanasiasa wanapolipwa zaidi kuliko yeyote.

Mwingine aliyejitambulisha kama HappinesslsFree, amehoji je? Tuendelee na watu kama Kibajaji au Msukuma kuamua juu maendeleo yetu?  

Eric Muganga katika hilo naye ameandika; Maprofesa na Madaktari wamechoka kuongozwa na watu wasio na uelewa, kwamba sasa wanataka madaraka ili kurudisha mfumo kwenye mstari unaotakiwa.

Dr. Dexter naye amekuwa na mtazamo tofauti kuhusu hoja hiyo ya Profesa Shivji anasema Maprofesa na Madaktari wanaona elimu zao haziwasaidii kuwapa heshima  au maslahi wanayostahili…pale wanapofikiria Msukuma yupo bungeni yeye yupo anasahihisha ‘assignment’ na anatungiwa sheria na mtu huyo wa elimu hiyo..sheria ambazo wakati mwingine zinakuwa za ovyo na huku mtu huyo akipata fedha nyingi.

Mugya yeye amejibu maswali ya Profesa Shivji akiandika; Maslahi ya ubunge 

1. Mshahara 3.8 kwa mwezi 

2. Posho mezi 8M

3.Posho kikao 240K

4. Kujikimu siku 120K

5. Pensheni 240M baada ya miaka 5

6.Bima  ya Afya daraja la kwanza wewe na familia.

7. Safari za nje

8.Mshahara bila makato ya Bima ya afya wala mfuko wa hifadhi ya jamii.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumza na MTANZANIA Jumamosi juzi alisema sababu za idadi kubwa ya watu kujitokeza ni kwamba CCM ni chama kubwa na kinapendwa na wengi. 

Je ni kweli CCM kinapendwa na wengi sasa? Hili ni swali jingine ambalo wengi wanajiuliza.

Miaka mitano iliyopita katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na hapo kabla, ukweli ni kwamba CCM ilipoteza mvuto kwa kiwango ambacho miaka mitano baadae pengine kingekuwa mahututi zaidi. 

Kilikuwa kimechafuka kutokana na taswira ya ufisadi, makundi, majungu, fitna, rushwa, kutotenda haki, kuminya demokrasia na mambo mengine kadha wa kadha.

Hoja hizo ambazo zilibebwa na upinzani na hata kufanikiwa kuvipa umaarufu na hasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakati huo si tu wale waliovaa sare za CCM waliona karaha kupita mitaani bali hata wauzaji wa nguo za chama hicho walikuwa wakizomewa na ilikuwa aibu.

Mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, mwaka 2015, ambaye baadae alishinda uchaguzi lakini huku kura zikipunguzwa na upinzani kwa kiwango kikubwa, katika wa kampeni za wakati huo, alikuwa akiogopa hata kutaja jina la chama hicho, zaidi alionekana kujibeba yeye mwenyewe kwa haiba yake ya uchapaji kazi na maamuzi magumu tangu akiwa Waziri wa ujenzi katika serikali za awamu ya tatu na nne.

Mtangulizi wa nafasi ya Polepole, Nape Nnauye alipata kukiri hadharani pale St. Peter’s, Dar es Saaam siku chache baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri wa Habari katika Serikali ya  Rais Magufuli mwaka mmoja baada ya uchaguzi, kwamba wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 CCM kilikuwa kinaelekea shimoni.

Kwamba walifanya kazi kubwa kukiokoa yeye na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na kuonyesha kuwa hata ushindi wa wakati huo ulikuwa ni wa tia maji tia maji. 

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, pengine kwa kulitambua hilo kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, alifanya mabadiliko kadhaa, ukiacha staili yake ya uongozi wa maamuzi magumu, ukweli mchungu ni kwamba Serikali yake imelaumiwa  kuvibana vyama vya upinzani ambavyo pamoja na matatizo ya vyama hivyo mengine kila kukicha sasa vinaonekana kujikongoja.

Pamoja na hilo alionekana kutumia kila njia kurudisha nidhamu na kutibu majeraha mengi ndani ya chama hicho na kuondoa dhana iliyoonekana kwa wengi kama CCM ni chama cha watu fulani au kuna watu ambao wako juu ya chama hicho.

Chini ya uenyekiti wake CCM, sisemi kama  ni sahihi au si sahihi imemfukuza aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye amekuwa akituhumiwa kwa makosa ya uadilifu na kuanza mbio za urais mapema.

Lakini pia ikiwapa karipio na baadae kuwasamehe mtu kama Kinana na kumuonya aliyekuwa Katibu Mkuu wake kabla ya Kinana, Mzee Yusuf Makamba ambao walikuwa wakituhumiwa kwa makosa ya uadilifu.

Lakini pia ameonekana akijitahidi kupunguza migawanyiko ndani ya chama hicho, na mfano mzuri ni jinsi chama hicho kilivyoendesha mchakato wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar, kwani wagombea wote waliitwa Dodoma na hawakukatwa juu juu kama ilivyokuwa huko nyuma. 

Hatua ya kumrudisha ndani ya CCM haijalishi njia aliyoitumia, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ilionekana si tu kutafuta nguvu iliyopotea bali kutibu majeraha ndani ya chama hicho.

Lowassa ambaye baada ya jina lake kukatwa kimizengwe ndani ya CCM  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alipohamia upinzani alifanikiwa kukipunguzia kura chama hicho kwa kiwango kikubwa na kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi nchini, CCM ilijikuta ikipoteza kura nyingi na viti vingi vya ubunge. 

Jambo jingine ni staili ya utendaji kazi wake na maamuzi makubwa aliyoyafanya katika kutekeleza miradi mikubwa mbalimbali ya maendeleo, kama ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la Rufiji wapo wanaoona kama kuna u-‘serious’ na si danadana tena. 

Juzi  wakati akiwaapisha viongozi aliowateua  kushika nafasi mbalimbali ikiwamo zile za waliochukua fomu za kuwania ubunge ndani ya CCM, Rais Magufuli alizungumza mambo makubwa mawili kuhusu wimbi kubwa la walijitokeza kuchukua fomu ndani ya CCM.

Kwanza alisema watu hao wameona CCM sasa kuna demokrasia, lakini pili alizungumzia tamaa  hasa upande wa watumishi  aliowateua  ambao wameamua kutoa sadaka nafasi zao na kugeukia ubunge. 

Kwa maneno yake mwenyewe Rais Magufuli alisema ni vizuri viongozi wakajifunza kuridhika na kutumikia vyema nafasi walizonazo. 

Alisema vijana wengi ambao ni viongozi ndani ya Serikali, wamekuwa hawaridhiki na nafasi walizonazo na kuwataka wajifunze kuridhika.

Alisisitiza hajamtuma mtu kwenda kugombea na kuwataka wanaCCM kuwapima wagombea kwa namna watakavyowafaa katika kuwawakilisha.

 “Katika kazi hizi kuridhika ni vizuri, yule kijana anaitwa Seleman ni ‘Phd holder’, lakini alikuwa anapata mshahara wa Sh 500,000, amefanya kazi yake makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi.

“Aliridhika kwa sababu kazi yake ilikuwa ni utumishi, ana Phd ameichukulia China, lakini karidhika na mshahara wa 500,000.

“Ilipojitokeza fursa tukamteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, sasa sifahamu unajua vijana saa nyingine hawaridhiki haraka haraka, hasa waliozaliwa miaka ya 1982, lakini ni matumaini yangu atakwenda kuitumikia kazi yake vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Kabla Rais Magufuli hajatoa kauli hiyo  mapema wiki hii alimwondoa  aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa siku moja baada ya kuchukua fomu ya kuomba kugombea ubunge katika Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexandar Mnyeti na hapo kabla ambaye aliondolewa hata kabla hajachukua fomu ya ubunge ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye naye ameomba kugombea ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kupitia CCM.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry yeye aliomba kustaafu nafasi hiyo na baadaye akachukua fomu ya kuomba kugombea ubunge katika Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro. 

Pamoja na kauli hiyo ya Rais Magufuli hata hivyo baadae iliongezeka idadi ya watumishi wengine walioamua kuacha nafasi zao na kujielekeza kwenye ubunge kupitia CCM.

Vigogo hao ambao Rais Dk. John Magufuli alianza kuwaondoa kwenye nafasi zao kabla na mapema wiki hii na wengine juzi ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi ambao wote wamekwishachukua fomu ya kuwania ubunge,

Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda.

Juzi hiyo hiyo Rais Magufuli alijaza nafasi nyingine tena mbali na hizo.

Mojawapo ya nafasi alizojaza saa chache baadae juzi  baada ya zile za akina Ole Sendeka ni pamoja na ile ya Katibu Tawala Mkoa wa Songwe iliyokuwa ikishikiliwa na mwanasiasa David Kafulila.

Nafasi ya Kafulila ilijazwa muda mfupi baada ya kuaga akieleza kuwa anaelekea kuwania ubunge katika jimbo la Kigoma Kusini ambalo alikuwa mbunge wake kabla ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Pia Rais Magufuli pia amemteua Mussa Chogelo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam akichukua nafasi ya Sophia Mjema ambaye naye anadaiwa kwenda kuwania ubunge wa viti maalum.

Wiki hii Rais Magufuli alikuwa na kibarua cha uteuzi, kwani wengine walioteuliwa ni pamoja na Aswege Kaminyonge kuwa Mkuu wa Wilaya Maswa mkoani Simiyu.

Kabla ya uteuzi huo, Kaminyonge alikuwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya na anachukua nafasi ya Dk. Seif Shekilage ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe.

Pia amemteua Calorius Misungwi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na anachukua nafasi ya Julieth Binyura.

Rais Magufuli pia amemteua Dk. Athuman Kihamia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Mwingine aliyeteuliwa ni Lainie Kamendu  ambaye amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Kabla ya uteuzi huo, Kamendu alikuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na anachukua nafasi ya Aloyce Kwesi.

Hanan Bafagil naye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha mkoani Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Bafagil alikuwa Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na anachukua nafasi ya David Kihenzile.

Huko nyuma CCM na hata Rais Magufuli mwenyewe amepata kuonya Wakuu wa Mikoa, wilaya, makatibu wakuu na watumishi wengine ambao watagombea ubunge akisema hatawaacha.

Lakini pamoja na hayo, viongozi hao wameonekana kuwa tayari kupoteza nafasi hiyo kwa kucheza mchezo wa pata potea na hoja kubwa inayoelezwa na wengi ukiacha ile ya kutumwa ambayo Rais Magufuli mwenyewe ameikana, wengine wanaona hali hiyo inachagizwa  na mambo mengi.

Mambo hayo ni maslahi duni katika sekta nyingine, tamaa ya kupata mafanikio haraka, watu kufuata maslahi makubwa, ulinzi wa kazi zao kwani kwa sasa ni rahisi kutumbuliwa iwapo utakosea.

Hoja kubwa na ambayo imeonekana kugusa wengine wengi waliojitokeza kusaka ubunge ndani ya CCM ni ile ya kutafuta nafasi ya kuteuliwa baada ya Uchaguzi Mkuu sasa hili wengi wanaona linagusa mbali na maslahi makubwa, pia tatizo la ajira ambalo linawakabili wengi kwani leo hii si aghalabu kukutana na kijana aliyemaliza digrii yake akawa bado hajapata ajira na hana cha kumwingizia kipato.

Wengi wenye ndoto hiyo wanakumbuka jinsi ambavyo Rais Magufuli amefanya uteuzi kwa wale waliokosa nafasi ya kuteuliwa baada ya kujitokeza kuwania ubunge,udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kama ndivyo hapa ndipo unapoweza kuona mantiki ya hoja kama zile za Richard Mabala kuhusu mfumo ambao unaonekana kwa upande wa maslahi kuwalipa zaidi wanasiasa kuliko watu wa sekta nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles