25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRA KUKUSANYA KODI YA MAJENGO BAADA YA UTHAMINI

Na KOKU DAVID- DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepewa mamlaka ya kusimamia na kukusanya kodi ya majengo tangu Julai mosi, mwaka jana kwa  mujibu wa  mabadiliko ya Sheria ya Majengo sura namba mbili ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura namba 290 na Sheria ya mamlaka ya mapato ya Tanzania  sura ya 339.

Kodi ya majengo ni tozo inayotozwa kwa mujibu wa sheria  kwenye majengo au nyumba ambazo zinakaliwa au kumilikiwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi  na sheria nyinginezo za nchi.

Pia majengo hayo au nyumba hizo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa kuwa zimefanyiwa uthamini, ikiwa ni pamoja na wamiliki wake kutambuliwa kwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Pamoja na tozo hizo, kuna baadhi ya majengo na nyumba zinazosamehewa kodi ya majengo kwa mujibu wa sheria.

Majengo yanayoweza kusamehewa kodi ni zile nyumba zinazotumika kwa matumizi ya rais, majengo yanayomilikiwa na kutumiwa na Serikali kwa matumizi ya umma, maktaba za umma na majengo ya makumbusho, majengo ya shughuli za meli na majengo yanayomilikiwa na Serikali.

Pia msamaha mwingine katika kodi za majengo hutolewa katika majengo yanayomilikiwa na asasi zisizo za kiserikali yasiyotumika kwa shughuli za biashara, kujipatia faida au kipato, majengo yoyote ambayo waziri mwenye dhamana ataamua kuyatolea tangazo kwenye gazeti la Serikali pamoja na nyumba ambayo inamilikiwa na mstaafu au anayoishi mlemavu ambaye hana  kipato chochote.

Kabla ya majengo au nyumba hizo kulipiwa, zinatakiwa kufanyiwa uthamini na kwamba uthamini huo ni mchakato unaofanywa ili kuweza kujua thamani ya jengo au nyumba kwa ajili ya kutoa madai sahihi ya  kodi ya majengo.

Katika mchakato wa uthamini, mamlaka za Serikali za mitaa zimepewa jukumu la kuchagua wathamini wa majengo ambao watatayarisha jedwali au orodha ya majengo au nyumba katika maeneo ya miji na manispaa zao.

Kwa upande wa TRA kwa kushirikiana na mamlaka ya Serikali za mitaa, pia watachagua wathamini kuwa mawakala kwa kutayarisha orodha au majedwali kwa ajili ya kutoza kodi ya majengo katika mamlaka za Serikali za mitaa husika.

Kwa mujibu wa sheria, mthamini wa majengo anatakiwa kuwa amesajiliwa na sheria ya wathamini wa majengo, awe ofisa mwajiriwa wa mamlaka ya utozaji kodi ya majengo pia awe ni ofisa wa Serikali katika idara  ya uthamini aliyeteuliwa na waziri husika.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema wakati wa uthamini taarifa zitakazohitajika ni jina  kamili la mmiliki, anuani  kamili au mawasiliano, namba  ya kiwanja au jengo, hati au leseni ya makazi, mwaka ambao jengo lilijengwa, gharama iliyotumika katika ujenzi au ununuzi na matumizi ya jengo husika iwapo ni makazi au biashara.

Anasema baada ya uthamini kila mmiliki atatakiwa kulipia jengo lake au nyumba kwa kutumia mfumo unaotumika kukusanya kodi ya majengo ambao una uwezo  wa kuandaa na kutoa hati ya madai ya kodi ya majengo ambayo mteja ataweza kulipia katika  benki yoyote ya kiabiashara.

Anasema mfumo huo wa benki umeunganishwa na mfumo  wa malipo ya kodi  RGS ( Revenue Gate System) na kwamba malipo hayo huonekana katika mfumo wa TRA.

Katika suala zima la ulipaji wa kodi za majengo, tozo hizo hutofautiana kutokana na sheria ndogo zilizotungwa na mamlaka za Serikali za mitaa husika na kwa upande wa maeneo ndani ya jiji moja tozo hutofautiana, pia tozo za ndani ya manispaa moja na mji mmoja hutofautiana.

Katika kuhakikisha zoezi la ulipaji wa kodi za majengo linafanikiwa, TRA imefanya tathmini ya majengo ili kuweza kuwa na viwango ambavyo ni rafiki, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za ukusanyaji wa kodi ya majengo, kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulipaji wa kodi ya majengo, kuhakikisha inashughulikia pingamizi za kodi ya majengo katika muda mwafaka pamoja na kuboresha daftari la jedwali au orodha ya uthamini ili kuwa na takwimu sahihi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles