26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

AFRIKA KUSINI YAHITAJI MAZAO YA KILIMO, SARUJI

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Afrika Kusini ukiongozwa na Rais Jacob Zuma, ulifanya majadiliano kati yao na  wafanyabiashara wa Tanzania kwa nia ya kushirikiana katika uwekezaji nchini.

Ilisemwa hivi sasa biashara kati ya Afrika Kusini na Tanzania imeimarika ambapo hadi kufikia mwaka huu, Afrika Kusini imeshirikiana na Tanzania katika miradi 22 yenye gharama ya Dola milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.2.

Baadhi ya wadau wa biashara kutoka Afrika Kusini, walisema uhusiano wa nchi hizi mbili ni wa kihistoria hivyo ni budi kuimarishwa kwa maendeleo ya uchumi na hasa sekta ya biashara na viwanda.

 Aidha, walihamasisha Watanzania kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuuza nchini mwao kwani lipo soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa Tanzania ili kuinua uchumi  kati ya nchi hizi mbili.

Akitoa mada yake, Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji Afrika Kusini Kitengo cha  Biashara na Viwanda, Zanele Mkhize, alielezea umuhimu wa kuwepo kwa mahusiano ya kiuchumi endelevu kati ya nchi hizo mbili.

Alisema kwa sasa biashara kati yao zimeimarika lakini bado idadi ya wawekezaji  Watanzania nchini  Afrika Kusini ni ndogo na kwamba ipo haja ya wengine kuwekeza nchini humo kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa nchi hizi mbili.

“Tanzania pia inazalisha na kuuza bidhaa nzuri lakini changamoto iliyopo ni kwamba bado inazalisha kwa kiwango kidogo sana, hivyo kupitia mkutano huu wawekezaji wataweza kujadiliana namna ya kuboresha bidhaa na uzalishaji kwa njia za kisasa zaidi ili kuweza kukidhi soko la kimataifa,” alisema Zanele.

Akaongeza kuwa Afrika Kusini kuna soko kubwa la bidhaa kama kahawa, chai, korosho na hivyo nchi hiyo iko tayari kusaidia Tanzania kuongeza thamani katika bidhaa hizo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Clifford Tandari, aliliambia MTANZANIA kuwa yapo maeneo ambayo wafanyabiashara hao wamekubaliana kuwekeza hasa sekta ya uvuvi ambapo wawekezaji watajenga viwanda katika ufukwe wa Bahari ya Hindi ambapo samaki watasindikwa na kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema mwitikio wa wawekezaji wa nchi zote mbili umekuwa mkubwa ambapo zaidi ya wafanyabiashara 400 walishiriki ambapo jumla ya miradi 100 inategemewa kuendelezwa kupitia ushirkiano kati ya wakezaji wa pande zote mbili.

Naye Mkurugenzi wa kukuza uwekezaji wa TIC, Zacharia Kingu, alisema wapo wawekezaji kutoka Afrika Kusini ambao wako tayari kuwekeza katika kilimo cha miwa ili kuongeza uzalishaji wa sukari ambao bado hautoshelelzi soko la ndani kwa sasa.

“Hadi sasa pamoja na kuwa na maeneo mengi na makubwa ambayo yanafaa kwa kilimo cha miwa nchini, bado hatujaweza kukidhi soko la ndani hivyo kutokana na ushirikiano huu wa kibiashara kati yetu, tatizo hilo litaondoka na tutaweza kukidhi soko la ndani na la nje pia,” alisema.

Akihutubia katika mkutano huo, Rais Zuma alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika nyanja za kibiashara kati ya nchi hizi mbili na akaongeza kuwa wakati umefika wa kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa kuhakikisha unashikiliwa na kushirikisha wananchi wa kipato cha chini.

“Nchi zetu zinatofautiana katika historia za kiutawala ambapo nchi yetu ilitawaliwa kwa miaka mingi na kusababisha wawekezaji wageni kujilimbikizia mali na kuanzisha biashara nyingi na kwa hilo imesababisha asilimia kubwa ya uchumi wa nchi kushikiliwa na matajiri wachache, tofauti na Tanzania, hivyo kilichopo sasa ni kufanya mabadiliko kiuchumi kwa kuhakikisha wananchi wa kipato cha chini ambao ndio tabaka la walio wengi wanashirikishwa kwa kiasi kikubwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili nao wanufaike na rasilimali zao,” alisema.

Akaongeza kuwa katika majadiliano waliyofanya na Rais Magufuli, zipo sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika kuziendeleza kwa njia ya uwekezaji zikiwemo sekta ya miundombinu, madini, uvuvi, kilimo, ujenzi wa reli, mawasiliano na pia utalii.

Naye Rais Dk. John Magufuli alisisitiza kuwa Tanzania ina aina nyingi za rasilimali ambazo zinatakiwa kuendelezwa kwa nia ya kuimarisha uchumi na akawasisitizia wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini kuchangamkia fursa hizo.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara wa Afrika ya Kusini, Dk. Rob Davies, alisema mapema kabla ya ujio wa Rais Zuma, walikuwa na mazungumzo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji nchini, Charles Mwijage, ambapo walikubaliana kushirikiana katika kuboresha biashara na viwanda na pia sekta mbalimbali. Alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na uoto ambao unalimwa mazao aina nyingi ambayo mengi yanahitajika nchini Afrika Kusini yakiwemo kahawa, korosho, mafuta ya kupikia na bidhaa kama saruji.

“Tutahakikisha tunatoa msaada wa kiufundi kwa rafiki zetu Watanzania, hasa katika kuongeza thamani za mazao na kilimo bora na cha kisasa ili kukidhi vigezo vya soko la kimataifa,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles