Na Shermarx Ngahemera
SERIKALI inasema haitozi kodi kubwa kwani viwango vyake ni vya kawaida kama nchi nyingine na inatafuta wawekezaji na hivyo itakuwa inajipinga yenyewe kwa kuweka kiwango kikubwa, Mtanzania inaweza kuandika.
Akizungumza na wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri (TEF) katika semina ya siku moja kwenye Chuo cha Kodi (ITA), Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi kwa Umma, Richard Kayombo, alisema watu wengi wanaodai kiwango cha kodi ni kikubwa ni wale ambao hawaweki taarifa sahihi za hesabu za biashara zao kwani wale wanaofuata taratibu hawalalamiki na wanalipa kodi bila shuruti.
“Tumesikia lawama hizo toka kwa wachache na tukiwadadisi wapi wameonewa au msingi wa malalamiko yao wanashindwa kutetea madai yao na hivyo kujua kuwa wanababaisha tu kwani kuna ngazi mbalimbali za kushughulikia matatizo ya kodi na inafuata miongozo ya kimataifa.”
Anasema kodi chini ya TRA ni ya wazi na shirikishi na inazingatia vigezo vyote vya uhalali na kukubalika kwani wao hawatungi kodi bali Bunge, ila wanasimamia sheria na taratibu na hivyo si rahisi kufanya kinyume na mahitaji yake.
“Cha ajabu kikubwa ni kuwa madai hayo yanaongelewa na wapambe na si walipa kodi wenyewe kwani kodi ina mambo mengi ikiwamo kuomba unafuu, kufutiwa madai, kuongezewa kiasi cha malipo na kupewa adhabu kwa makosa mbalimbali na hivyo ni mfumo wenye kujitegemea na kujidhibiti yaani una ‘checks and balances,” alisema Kayombo.
Kuhusu madai kuwa kodi hazieleweki, Kayombo alisema si kila mtu anaweza kuzungumzia masuala ya kodi kwani ni taaluma kama taaluma nyingine inabidi ubobee katika masuala yake ambayo inawahusu vile vile wanasheria na wahasibu ili kuelewa mambo kwa ujumla wake na kutoa mawasilisho.
Hivyo lazima watu na hasa taasisi watumie huduma za wajuzi wa masuala ya kodi kwa kuwasilisha taarifa sahihi kwenye mamlaka, vinginevyo utafanya makosa na kulipa zaidi au kupewa adhabu kwakutokuzingatia mwenendo na taratibu.
Wafanyakazi wa TRA wao lazima wawe na leseni ya kufanyia kazi na huambatana na kufanya mafunzo na mitihani kama taaluma nyingine zinavyotaka.
Alitupilia mbali madai katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa wawekezaji wanakimbia kutokana na kodi kubwa na ubabaishaji wakati wa kushughulikiwa masuala ya kodi.
Alisema madai hayo ni uongo kwani kuna mamlaka na vigezo vingi vinavyozingatiwa na wawekezaji na si kodi pekee na hivyo wao hufuata pale ambapo ni tija kwao ipo na si udogo wa kodi kwani hawalipi wao binafsi bali kampuni zao na hivyo usumbufu haupo.
Reuters ilidai mwezi uliopita kuwa kuna kampuni sita kubwa bila kuzitaja kwa majina zilikuwa zinafunga ofisi au kupunguza shughuli zao kutokana na kubanwa na masuala ya kodi.
Reuters ilisema makampuni iliyowahoji ni yale kutoka sekta ya madini, mawasiliano, masuala ya usafiri wa meli na kilimo.
Kayombo anasema kuwa sasa hivi nchi ina ajenda mahususi ya kufikia uchumi wa viwanda kuwa nchi ya daraja la kati na na ina malengo mwafaka wa ukusanyaji kodi ambapo zinatakiwa kukusanywa shilingi zaidi ya trilioni 29 mwaka huu na TRA imepewa lengo la shilingi trilioni 15 takribani asilimia 54 ya mahitaji na hivyo kuimarisha shughuli ya ukusanyaji kutoka bilioni 850 kwa mwezi hadi trilioni zaidi ya 1.2 kwa mwezi.
Rais Dk. Magufuli amekuwa muwazi juu ya dhamira ya nchi kuwa ya viwanda na hivyo inahitaji juhudi ya ziada ya taasisi za Serikali kufanya shime ili azma hiyo iweze kufikika na kupatikana kama ilivyokusudiwa na ulipaji kodi ni nyenzo muhimu kufikia malengo rasmi.
Mabadiliko ya kodi
Katika kutekeleza majukumu yake TRA imefanya mabadiliko kadhaa kuwezesha na kuhamasisha ukusanyaji kodi.
Takwimu za makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 inaonesha Serikali ilikusanya shilingi trilioni 9.8 au dola bilioni 4.5 na kwa mwaka 2016/2017 lengo ni kukusanya shilingi trilioni 15.1 ongezeko la ziada ya zaidi ya asilimia 50 na hivyo kuleta sokomoko mitaani na kuleta manung’uniko kuwa kodi imepanda wakati viwango bado ni vile vile na sehemu nyingine kupunguzwa au kufutwa.
Cha maana kujua ni kuwa wale wote wahusika wa mradi mkubwa wa uwekezaji wa dola bilioni 30 wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia utakaojengwa pale Likong’o, Lindi hakuna aliyejitoa na hivyo kuhakikishia Watanzania maisha bora ya baadaye na ule mradi wa dola bilioni 3 wa mbolea utakaojengwa na nchi za Ujerumani na Denmark unaendelea kiutekelezaji.
Uwekezaji wa moja kwa moja toka nje ni mkubwa sana Tanzania ukifananisha na nchi nyingine kutokana na kupata kiwango cha dola zaidi kidogo ya bilioni 1.5 kwa mwaka jana kwa uchumi wenye uwezo wa dola bilioni 45 kama lilivyoainisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Uwekezaji (UNCTAD) na Benki ya Dunia.
Urasimu na rushwa ndio matatizo makubwa Tanzania na hivyo kumfanya Rais Magufuli kuweka mbele vita dhidi ya mambo hayo kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.
“Utawala wa kodi umeimarishwa kwa kuunda upya taasisi ya TRA na kuanzisha Utawala Mpya wa Masuala ya Kodi (Tax Administration Act 2015) na kupanua wigo wa kodi kwa kuanzisha kodi mpya ikiwamo ile ya kuhusu miamala ya fedha kupitia simu za mkononi na benki, kodi ya ongezeko la thamani kwenye utalii na gharama za huduma kwa mizigo inayopita (transit),” inaonesha bajeti ya mwaka huu.
Serikali inasema hayo ni mambo ya mpito tu kwani baada ya matumizi itapatikana mwafaka wa mambo kwani faida zake ni za wazi kwani zitakuza biashara na hivyo uchumi na watu kuneemeka baada ya muda.
Adolf Mkenda ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anasema malalamiko yamesikika lakini sera ya nchi ni ya wazi na inataka pande zote kuneemeka na hivyo Serikali huneemeka kwa kupata kodi na si vinginevyo.
TRA kuonesha iko sahihi imeshinda kesi 9 kati ya 10 zilizopelekwa mahakamani wakati Mkurugenzi Kayombo anaainisha kuwa kodi inahitajika kwa kugharamia miradi ya miundombinu kwa ajili ya uchumi wa viwanda ikiwamo umeme, maji, barabara, reli na bandari.