27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: KODI SI TATIZO BALI WALIPA KODI 

Na Shermarx Ngahemera


richard-kayomboSERIKALI inasema haitozi kodi kubwa  kwani viwango vyake ni vya kawaida kama nchi nyingine na inatafuta wawekezaji na hivyo itakuwa inajipinga  yenyewe kwa kuweka kiwango kikubwa,  Mtanzania inaweza kuandika.

Akizungumza na wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri (TEF) katika semina ya siku moja kwenye Chuo cha Kodi  (ITA), Mkurugenzi  wa Elimu ya Kodi kwa Umma, Richard  Kayombo, alisema watu wengi wanaodai kiwango cha kodi ni kikubwa ni wale ambao hawaweki taarifa sahihi za hesabu za biashara zao kwani wale wanaofuata taratibu hawalalamiki na wanalipa kodi bila shuruti.

“Tumesikia lawama hizo toka kwa wachache na tukiwadadisi wapi wameonewa au msingi wa malalamiko yao wanashindwa  kutetea madai yao na hivyo kujua kuwa wanababaisha tu kwani kuna ngazi mbalimbali za kushughulikia matatizo ya kodi na inafuata miongozo ya kimataifa.”

Anasema kodi chini ya TRA ni ya wazi na shirikishi  na inazingatia vigezo vyote vya uhalali na kukubalika kwani  wao hawatungi kodi bali  Bunge, ila wanasimamia sheria na taratibu na hivyo  si rahisi kufanya kinyume na mahitaji yake.

“Cha ajabu kikubwa ni kuwa madai hayo yanaongelewa na wapambe na si walipa kodi wenyewe kwani kodi ina mambo mengi ikiwamo kuomba unafuu, kufutiwa madai, kuongezewa kiasi cha malipo na kupewa  adhabu   kwa makosa mbalimbali na hivyo ni mfumo wenye kujitegemea na kujidhibiti yaani una ‘checks and balances,” alisema Kayombo.

Kuhusu madai kuwa kodi hazieleweki, Kayombo alisema si kila mtu anaweza kuzungumzia masuala ya kodi kwani ni taaluma  kama taaluma nyingine inabidi ubobee katika masuala  yake ambayo inawahusu vile vile wanasheria na wahasibu  ili kuelewa mambo kwa ujumla wake na kutoa mawasilisho.

Hivyo lazima watu  na hasa taasisi watumie huduma za wajuzi  wa masuala  ya kodi kwa kuwasilisha taarifa sahihi kwenye mamlaka, vinginevyo utafanya makosa na kulipa zaidi au kupewa  adhabu kwakutokuzingatia mwenendo na taratibu.

Wafanyakazi wa TRA wao lazima wawe na leseni ya kufanyia kazi na huambatana na kufanya mafunzo na mitihani kama taaluma nyingine zinavyotaka.

Alitupilia mbali madai katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa wawekezaji wanakimbia kutokana na kodi kubwa na ubabaishaji wakati wa kushughulikiwa  masuala ya kodi.

Alisema madai hayo ni uongo kwani kuna mamlaka na vigezo vingi vinavyozingatiwa na wawekezaji na si kodi pekee na hivyo  wao hufuata pale ambapo ni tija kwao ipo na si udogo wa kodi kwani hawalipi wao binafsi  bali kampuni zao na hivyo usumbufu haupo.

Reuters ilidai mwezi uliopita kuwa kuna kampuni sita  kubwa  bila kuzitaja kwa majina zilikuwa zinafunga ofisi au kupunguza shughuli zao kutokana na kubanwa  na masuala ya kodi.

Reuters ilisema makampuni iliyowahoji ni yale kutoka sekta ya madini, mawasiliano,  masuala ya usafiri wa meli na kilimo.

Kayombo anasema kuwa sasa hivi nchi ina ajenda mahususi ya kufikia uchumi wa viwanda  kuwa nchi ya daraja  la kati na  na ina malengo mwafaka wa ukusanyaji kodi ambapo  zinatakiwa kukusanywa  shilingi zaidi ya trilioni 29 mwaka huu  na TRA  imepewa lengo la shilingi trilioni 15 takribani asilimia 54  ya  mahitaji na hivyo kuimarisha  shughuli ya ukusanyaji  kutoka bilioni 850 kwa mwezi hadi trilioni zaidi ya 1.2 kwa mwezi.

Rais  Dk. Magufuli  amekuwa muwazi juu ya dhamira ya nchi kuwa ya viwanda na hivyo inahitaji juhudi ya ziada ya taasisi za Serikali kufanya shime ili azma hiyo iweze kufikika na  kupatikana kama ilivyokusudiwa  na ulipaji kodi ni nyenzo muhimu  kufikia malengo rasmi.

Mabadiliko ya kodi

Katika kutekeleza majukumu yake TRA imefanya mabadiliko kadhaa kuwezesha na kuhamasisha ukusanyaji kodi.

Takwimu za makusanyo ya kodi  kwa mwaka  wa fedha  2014/2015  inaonesha Serikali ilikusanya  shilingi trilioni 9.8 au  dola bilioni  4.5 na kwa mwaka 2016/2017 lengo ni  kukusanya  shilingi  trilioni 15.1  ongezeko la ziada ya zaidi ya asilimia 50  na hivyo kuleta sokomoko mitaani na kuleta  manung’uniko kuwa kodi imepanda wakati viwango bado ni vile vile  na sehemu nyingine kupunguzwa au kufutwa.

Cha maana kujua ni kuwa wale wote wahusika  wa  mradi mkubwa wa  uwekezaji wa dola bilioni 30 wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia utakaojengwa pale Likong’o, Lindi  hakuna aliyejitoa na hivyo kuhakikishia Watanzania  maisha bora ya baadaye na ule mradi wa dola bilioni 3 wa mbolea utakaojengwa na nchi za Ujerumani na Denmark unaendelea kiutekelezaji.

Uwekezaji  wa moja kwa moja toka nje  ni mkubwa  sana  Tanzania ukifananisha na nchi nyingine  kutokana na  kupata kiwango  cha dola  zaidi kidogo ya bilioni 1.5 kwa mwaka jana kwa uchumi wenye uwezo wa dola bilioni 45  kama lilivyoainisha Shirika la Umoja wa Mataifa la   Biashara na Uwekezaji  (UNCTAD) na Benki ya Dunia.

Urasimu na rushwa ndio  matatizo makubwa Tanzania na hivyo kumfanya Rais Magufuli kuweka mbele vita dhidi ya mambo hayo kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.

“Utawala wa kodi umeimarishwa kwa kuunda upya taasisi ya TRA na kuanzisha Utawala  Mpya wa Masuala ya Kodi (Tax Administration  Act 2015) na   kupanua wigo wa kodi kwa kuanzisha  kodi mpya ikiwamo ile ya kuhusu miamala ya fedha kupitia simu za mkononi  na  benki, kodi ya ongezeko la thamani  kwenye  utalii na gharama  za huduma kwa mizigo inayopita (transit),” inaonesha bajeti ya mwaka huu.

Serikali inasema hayo ni mambo ya mpito tu kwani baada ya  matumizi  itapatikana mwafaka wa mambo kwani faida zake ni za wazi kwani zitakuza biashara na hivyo uchumi na watu kuneemeka baada ya muda.

Adolf Mkenda ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji  anasema malalamiko yamesikika lakini sera ya nchi ni ya wazi na inataka pande zote kuneemeka  na hivyo Serikali huneemeka kwa kupata kodi na si vinginevyo.

TRA kuonesha iko sahihi imeshinda kesi 9 kati ya 10 zilizopelekwa mahakamani  wakati  Mkurugenzi Kayombo anaainisha kuwa  kodi inahitajika kwa kugharamia miradi ya miundombinu kwa ajili ya uchumi wa viwanda ikiwamo umeme, maji,  barabara, reli na bandari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles