26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

TRA Arusha yataja sababu yakushindwa kufikia lengo

Na Janeth Mushi, Arusha

Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Mkoa wa Arusha, imesema moja ya sababu za kushindwa kufikia malengo ya makusanyo kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021 ni pamoja na athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu ya corona (Covid 19).

Aidha, kutokana na athari za mlipuko huo umesababisha biashara 917 kufungwa mkoani Arusha na kusababisha kuathiri makusanyo ya kodi ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani (VAT), PAYE, SDL na kodi za mapato.

Kauli hiyo imetolewa jana Januari 20, jijini hapa na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, John Mwigura, akiwasilisha taarifa ya makusanyo ya mapato kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/21 katika kikao cha kamati ya ushauri wa Mkoa (RCC).

Amesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita(Julai-Desemba) kwa mwaka wa fedha 2020-2021, TRA ilikusanya Sh bilioni 162.8 kati ya Sh bilioni 237.9 zilizotarajiwa kukusanywa sawa na asilimia 68 na kwamba makusanyo hayo hayahusiani na maduhuri ya serikali yatokanayo na utalii (non tax revenue).

Amesema kushuka kwa makusanyo kumechangiwa na mdororo wa kiuchumi uliosababishwa na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid 19, hasa ikizingatiwa shughuli nyingi za kibiashara mkoani humo hutegemea utalii.

“Sababu za kutokufikia malengo ya ukusanyaji ni pamoja na athari za mlipuko wa Covid-19¬†ambao umesababisha kufungwa kwa biashara¬†917 katika kipindi hicho, kushuka kwa makadirio ya kodi ambapo walipa kodi zaidi ya 2,000 walipunguza makadirio yao ya kodi ya mapato kutoka Sh bilioni 20.6 hadi kufikia Sh bilioni 10.6,”amesema Mwigura.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni kupungua kwa malipo ya VAT kutoka Sh bilioni 71.1 hadi Sh bilioni 39.7 madeni sugu ya kodi, hali ya matumizi ya EFD, kushuka kwa mzunguko wa fedha, usimamizi wa kodi kwenye vitalu (block management) pamoja na magendo kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini(Forodha).

Meneja huyo ametaja mikakati ya kuongeza makusanyo kwa kipindi cha nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2021/22 kuwa ni pamoja na kuongeza mikakati ya kutoa elimu kwa mlipakodi, kufuatilia matumizi sahihi ya mashine za EFD, ufuatiliaji wa madeni sugu, ufuatiliaji wa kodi za majengo na mabango, kuendesha doria maeneo ya mipakani na kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi.

Akichangia hoja hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima amesena wakishirikiana na kuanzisha kampeni ya kuhamasisha elimu ya masuala ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wananchi itasaidia kukuza mapato ya TRA na Halmashauri.

“Tuwe na mpango wa kuhimiza watu wanapoenda kununua vitu madukani wadai risiti hicho kitu kwa Arusha ni kikubwa sana kuna bei za risiti na ambazo siyo za risiti, kuna maduka wanakwambia nikikuuzia mfuko wa saruji na kukupa risiti ya serikali bei ni hii na nikikuuzia bila risiri bei ni tofauti,” amesema.

Aidha, ameshauri eneo linalotumika kwa ajili ya maonyesho ya Nanenane, kutumika kuongeza mapato kwa kipindi ambacho siyo cha maonyesho na kuwa waangalie miradi inayoweza kuwekwa katika eneo hilo bila kuwa na kikwazo chochote na washirikiane na wadau wengine katika kufanikisha hilo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kwani TRA wanakusanya mapato? Sehemu kubwa ya kodi huwa inakusanywa na walipaji na kuwasilishwa kiletroniki katika akaunti ya TRA bila hata TRA kujua . Mfano kila unapoweka fedha benki au unapotoa au unapouliza salio kuna VAT ambayo hukatwa na kuwasilishwa TRA (programmed). Halikadhalika katika utumiaj na upokeaji wa fedha kupitia Tigo au Airtel n.k. hata unapouliza salio unakatwa kodi – yote haya ni programmed
    Bado kuna malaki ya watumishi ambao mishahara yao hukatwa PAYE na fedha huwasilishwa TRA. Bado kuna manunuzi ambayo hukatwa VAT kiiletroniki –
    Hii ni mifano michache – katika yote haya TRA inafanya kazi gani? Labda kuhesabu fedha zilizozwasilishwa na kuwabana wasiowasilisha
    Pita Kariakoo na kuona wafanyabiashara wangapi wanatoa risiti – Labda asilimia moja tu – Hao mnaowaita wamachinga kuna wanaofanya biashara ya milioni moja na zaidi kwa siku lakini kodi yao ni sh 20,000 tu kwa mwaka

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles