Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimeunga mkono kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ya kuwataka polisi kutoa dhamana kwa mtuhumiwa wakati wowote bila kujali siku ya mapumziko wa mwisho wa wiki.
Pia kimesema kiko tayari kumuunga mkono katika kutoa mafunzo kwa watendaji wa Jeshi la Polisi ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na kuzingatia haki za binadamu na miongozo ndani ya jeshi hilo haswa amri ya mkuu wa polisi.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 2, na Rais wa chama hicho, Fatma Karume, amri hizo ni zile ambazo zinajieleza vizuri kwa kuzingatia haki za binadamu za jinsi ya kumkamata mtuhumiwa, kumweka kizuizini, kufanya upekuzi na uchunguzi.
Aidha, amesema chama hicho kinamshauri Waziri Lugola kutoa waraka wa serikali juu ya haki hiyo ya dhamana kwa polisi wote ili kukazia hitaji hilo muhimu la sheria ambalo limekuwa likikiukwa na baadhi ya watendaji wa wizara yake kwa miaka mingi sasa.
“Katika mkutano wa hadhara Jumapili Septemba 30, mwaka huu, waziri alieleza msimamo wa sheria juu ya haki ya mtuhumiwa kupata dhamana akiwa kituo cha polisi, msimamo huo umekuwa ukikiukwa kwa miaka mingi na baadhi ya polisi hapa nchini kwa visingizio mbalimbali.
“Chama kinaunga mkono msimamo wa waziri katika kusimamia, kutetea na kuishi msingi wa sheria na kinawashauri viongozi wengine wa serikali kuiga mfano huo mzuri,” imesema taarifa ya rais huyo.
Pamoja na mambo mengine, amesema kwa mujibu wa misingi ya kimataifa ya sheria ya jinai haswa nchi za jumuiya ya madola, makosa ya jinai ambayo hayana dhamana ni yale yenye adhabu ya kifo au kifungo cha maisha.
“Hata hivyo, kutokana na mabadiliko mbalimbali ya sheria za jinai hapa nchini makosa yasiyokuwa na dhamana yameongezeka ni pamoja na uhaini, mauaji, unyang’anyi wa silaha, uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, ugaidi na uasi ndani ya jeshi la wananchi,” amesema Fatma.