WASHINGTON: Marekani
MGOMBEA urais wa Marekani kwa chama cha Democrat, Hillary Clinton amemtaja senata wa zamani wa Virginia, Tim Kaine, kuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kaine akiwa mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa senate wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa, Hillary anamuamini kuwa anaweza kumsaidia katika kupata ushindi dhidi ya mpizani wake Donald Trump wa chama cha Republican.
Hillary alitumia chaguo lake hilo njia ya ujumbe mfupi katika mtandao wa jamii wa tweeter.
Habari zinasema Hillary aliamua kumteua Kaine (58) kwa vile ana sifa na historia nzuri.
Wengine ambao walionekana kama wangefaa katika nafasi hiyo ni Waziri wa Kazi, Thomas Perez na Senata Cory Booker wa jimbo la New Jersey, Mmarekani mwenye asili ya Afrika wa kwanza kutafuta nafasi ya makamu wa rais.
Mwingine ni James Stavridis, mwanjeshi mstaafu ambaye pia alikuwa kamanda wa kikosi cha majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Ulaya Magharibi (NATO).
Kwa maelezo ya Hillay, yeye na Kaine walikuwa wanasheria kabla hawajaingia kwenye siasa na walihitimu shule ya sheria katika Chuo Kikuu cha Harvard.
Aliliambia shirika la habari la PBS kuwa aliepuka kuchukua mtu mwenye uzoefu mdogo kama mgombea mwenza na pia hakutaka kumtafuta mwanamke mwingine katika nafasi hiyo.
Baada ya Hillary kutangaza mgombea mwenza, timu ya kampeni ya Donald Trump, moja kwa moja ikadai kuwa Kaine ni mla rushwa na kuwa alipokea zawadi alipokuwa gavana wa Jimbo la Virginia.
Msemaji wa Trump, Jason Miller, alisema haina maana kwa Hillary kumteua mtu ambaye hana madili, kwa mujibuwa gazeti la New York Times.
Trump amekwisha kumteua Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence kuwa mgombea mwenza wake katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba.