31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tibaijuka kutojiuzulu CCM

Profesa Anna Tibaijuka
Profesa Anna Tibaijuka

ALIYEKUWA Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema hayuko tayari kujiuzulu ujumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kumfuta kazi katika mkutano wake na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika Desemba 22, mwaka huu.
Tibaijuka alifutwa kazi kutokana na kukiuka maadili ya uongozi, baada ya kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh bilioni 1.6 zikiwa ni sehemu ya fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Msaidizi Kazi Maalumu wa Profesa Tibaijuka, Nassoro Hussain, alisema suala la Profesa Tibaijuka kujiuzulu nafasi yake ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM lipo chini ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, ambao wao ndio watakaoamua.
“Profesa Tibaijuka hayupo tayari kujiuzulu kwa sasa ujumbe wa Kamati Kuu, anachosubiri ni uamuzi wa chama. Jambo hili bado lipo kwa wakubwa na ni siri kwa kuwa lipo kiutendaji, hivyo litaamuliwa na Kamati Kuu ya chama,” alisema.
MTANZANIA ilipomtafua Profesa Tibaijuka ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini, ili kujua msimamo wake kuhusu kauli hiyo ya katibu wake, alipokea simu na alipoulizwa akamtaka mwandishi kukata na kupiga tena kutokana na kile alichodai tatizo la mawasiliano.
“Unaweza kukata na kupiga tena maana sikusikii kwa sasa,” alisema Profesa Tibaijuka.
Hata baada ya kupigiwa tena kama alivyoelekeza, simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Juzi Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, aliiambia MTANZANIA kuwa hatima ya Profesa Tibaijuka ya kukiuka maadili ya uongozi iko mikononi mwa Kamati Kuu ya chama hicho.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa awali ambao chama kimechukua dhidi ya Profesa Tibaijuka, Mangula alisisitiza kuwa kikao cha Kamati Kuu ndicho kilicho na mamlaka ya kutoa uamuzi wa jambo hilo.
Desemba 22, mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza kutengua uteuzi wa Profesa Tibaijuka huku akimuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusubiri taarifa alizoagiza zitafutwe.
Rais Kikwete pia alisema ameziachia mamlaka husika zifanye uchunguzi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na wakibaini kuwapo kwa makosa wamchukulie hatua, na siku mbili baadaye Ikulu kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilitangaza kumsimamisha kazi kupisha uchunguzi.
Hatua ya Rais Kikwete ilitokana na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge yaliyotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), juu ya ukaguzi wa miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow ambayo pamoja na mengine ilipendekezwa kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya viongozi wa umma waliotajwa kuhusika katika ukwapuaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti hiyo.
Desemba 18, mwaka huu katika mkutano wake na waandishi wa habari, Profesa Tibaujuka alisema hayuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri kwa kuwa hajaona kosa alilotenda na wala kwake kujiuzulu si fasheni.
Tibaijuka alisema suala la kujiuzulu kwake lingeweza kusababisha madhara ambayo yasingekuwa kwa Tanzania pekee bali hata kwa Umoja wa Mataifa (UN), ambako aliwahi kufanya kazi.
Alisema anaona fahari na wala si fedheha kupata mchango wa shule shilingi bil 1.6 kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila ambaye alimtaja kuwa ndugu yake, anayehusishwa na kufanya kazi ya kugawa fedha hizo kwa kutumia Benki ya Mkombozi.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alilazimika kujiuzulu kutokana na sakata hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles