24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wateketeza maduka, nyumba Tanga

pg1

NA AMINA OMARI, HANDENI
NYUMBA nane na maduka 30 vimeteketea kwa moto baada ya gari la mafuta lenye namba za usajili T 870 NFB kugonga nguzo ya umeme na mafuta kumwagika hali iliyosababisha kulipuka kwa moto.
Moto huo ulitokea jana katika eneo la Kivesa, barabara ya kuelekea Songe wilayani Handeni.
Imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliosababisha lori hilo kupinduka na mafuta kumwagika jirani na makazi ya watu kabla ya kuanza kusambaa barabarani.
Wakizungumza na MTANZANIA, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema kutokana na mwendo kasi, dereva wa lori hilo alishindwa kuhimili kona kali iliyopo kwenye eneo hilo na kugonga nguzo ya umeme.
“Baada ya lori hilo kuanza kuserereka, liliwaka moto huku mafuta yaliyokuwa kwenye tanki yakimwagika na kusambaa kwa kasi kwenye nyumba na maduka ya watu,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Nyoso Mwankale.
Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi walilazimika kuanza kuuzima moto huo ili usiweze kuleta madhara makubwa.
Gari la Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji liliwasili kwenye eneo hilo baada ya saa moja kupita, huku bidhaa zilizokuwa katika maduka hayo zikiteketea kwa moto.
Baada ya kuonekana kwa gari hilo, wananchi wenye hasira walianza kurusha mawe kwa askari wa kikosi hicho, huku gari likivunjwa vioo kwa kuchelewa kufika kwenye eneo la tukio.
Hali hiyo ilililazimu Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi na kufyatua risasi hewani kutawanya wananchi hao ambao tayari walikuwa wameshafanya uharibifu ikiwamo kuvunja vioo vya gari hilo.
Wananchi hao walisema kuwa wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya zimamoto na uongozi wa wilaya kushindwa kufika kwa wakati kwenye eneo la tukio ili kuweza kusaidiana kuzima moto huo.
Wakati tukio hilo likiendelea, baadhi ya vibaka walivamia maduka yaliyokuwa jirani na eneo hilo na kuanza kupora mali za wafanyabiashara huku wamiliki wakishindwa la kufanya.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alithibitisha kutokea kwa moto huo na kwamba juhudi zinafanywa kuudhibiti usilete madhara zaidi.
“Ni kweli moto unawaka, kwa sasa hatuwezi kusema kwamba ni athari kiasi gani imetokea, kinachofanyika ni kushirikiana na wenzetu wa Jeshi la Zimamoto kuudhibiti moto huo ili kuweza kuepusha madhara zaidi,” alisema.
Aidha Muhingo alitaja baadhi ya mali zilizoteketea ni gari aina ya Canter yenye namba za usajili T 615 BBE, pikipiki ya miguu mitatu aina ya Toyo yenye namba za usajili T 224 BCK na banda la kuku likiwa na kuku 30.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraser Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa kamili kuhusu tathimini ya athari zilizotokea ataitoa baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles