22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Nyalandu atangaza kugombea urais

Pg 3.

 

Na Kulwa Karedia, Singida
MBIO za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimechukua sura mpya baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kutangaza rasmi nia ya kugombea urais mwaka 2015.
Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wapigakura wake kwenye uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Ilongero, Wilaya ya Singida Vijijini jana, Waziri Nyalandu alisema muda wa Tanzania kupata maono mapya umefika.
“Muda wa Tanzania kupata maono mapya umefika, nitachukua hatua ya kuelekea Dodoma kuchukua fomu muda ukifika, maelfu ya watu watanisindikiza, wanawake, vijana kutoka mikoa mbalimbali.
“Naita zama mpya, siku ambayo ndoto yangu itakamilika, Mungu atanyanyua vyombo na kushangaza wakubwa. Najua tulikuwa wadogo kama Nazareti, lakini Ilongero imekuwa na mchango mkubwa ambao utakuwa si faida kwa wana Singida tu, bali taifa zima la Tanzania,” alisema Waziri Nyalandu.
Alisema kila mtu ambaye ametangaza nia ya kuwania urais ndani ya CCM, lazima kazi zake zipimwe kwa moto.
“Wale wote waliotangaza nia ndani ya chama chetu, kazi zao lazima zipimwe kwa moto na zianikwe hadharani ili mwisho wa siku CCM yenyewe itazipima,” alisema.
Alisema pindi Rais Jakaya Kikwete atakapohitimisha utawala wake, lazima atakabidhi kijiti kwa kizazi kipya.
“Nina uhakika mheshimiwa Rais Kikwete akiondoka madarakani, lazima akabidhi kijiti kwa kizazi chenye fikra… zama za kusimama na kuchukua vijiti zimefika.
“Mwaka 2015, sisi ndani ya CCM tunatarajia utakuwa mwaka wa mabadiliko na fikra mpya.
“Tuna wajibu wa kubadili fikra zetu, watu wasimamie Tanzania kuchukua hatua, licha ya ukweli kwamba CCM tuna utaratibu na itikadi zetu, tumeondoa zuio kwa vijana wasiwe waoga… tumejipanga kuwashangaza wengi,” alisema Waziri Nyalandu.

WAPINZANI
Alisema muda wa kuwashangaza wengi unaanzia kwa vyama vya upinzani, vikiwamo Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Katika safari ya miaka 15, Mungu ametusaidia kusonga mbele, safari moja huanzisha nyingine, nawaomba tusonge tena kwa hatua nyingine, mlianzisha safari yangu ya kisiasa, nilikuwa kama mzabibu uliotoa matunda, mkaniita ‘Mwanyengu’, maana yake mtoto wa tai la kuishangaza dunia. Safari hii imekuwa ya milima na mabonde lakini kwa pamoja tumeweza, Mungu ameona, Kikwete ameona sawasawa,” alisema.

VIONGOZI WAZEE
Alisema viongozi wastaafu waliotawala taifa hili wanapaswa kupewa heshima zote.
“Tunatambua mchango wa wazee wetu walioutoa, wana haki ya kuheshimiwa, lakini zamu ya vijana imefika. Vijana tunataka taifa litakaloleta siku njema, ni wajibu wetu tuwatunze ndiyo maana kupitia kwao maisha yetu yamebadilika,” alisema.
Alisema bado anawapenda mno wananchi wa jimbo lake, lakini safari waliyoianza mwaka 2000, lazima waikamilishe.
“Nalipenda jimbo langu, wapiga kura wangu, lakini tuungane kukamilisha safari hii tuliyoianza miaka 15 iliyopita,” alisema Waziri Nyalandu.

ATOA MAMILIONI
Baada ya kuwasili katika Kijiji cha Ilongero, Nyalandu alikwenda moja kwa moja katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ilongero ambako alishiriki misa na kuchangia Sh milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa.
Katika misa hiyo, alipewa nafasi ya kuzungumza na kusema eneo hilo ni la ushindi kwake.
Pia alitembelea Kanisa la FPTC-Tanzania ambako nako alitoa msaada wa Sh milioni 10 na kiasi kama hicho alitoa kwenye msikiti.
Katika mkutano huo, Nyalandu aliambatana na mke wake Faraja Kota, watoto wake Christopher na Serafine na wazazi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles