Na Editha Karlo
MBUNGE wa   Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) amewaeleza wapiga kura wake sababu ya kukataa  tuzo ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mamilioni ya fedha kuwa sheria za nchi haziruhusu kiongozi kupokea zawadi.
Profesa Tibaijuka aliyasema juzi kwenye mkutano  wa hadhara na wapiga kura wale uliofanyika  kwenye Viwanja vya Red Cross Muleba.
Alisema tuzo hiyo ya heshima ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili na UN ilikuwa ni kwa ajili ya kuthamini mchango wa kazi alizozifanya.
Mbunge huyo alisema   kukataa fedha hizo ni kukwepa mtego kama wa  mwaka juzi katka suala la Tegeta Escrow ambako alipata mgao wa Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mfanyabiashara wa Kampuni ya VIP.
“Mimi nina marafiki wengi   ndani ya nchi na hata nje ya nchi ambao wanapenda kazi zangu ninazofanya na wapo tayari kunichangia.
“Hizo fedha za tuzo wanazosema nimezikataa hazina tofauti na hela za Rugemalira tena zile ni mbaya zaidi,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema tuzo hiyo ilikuwa na vipengele vitatu ambavyo ni cheti, kikombe na   dola 100,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 200)
.Alisema alikataa  kuzipokea kwa sababu   ya sheria za nchi zilivyo sasa kwa viongozi hawaruhusiwi kupokea zawadi.