
Na Editha Karlo
MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) amewaeleza wapiga kura wake sababu ya kukataa tuzo ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mamilioni ya fedha kuwa sheria za nchi haziruhusu kiongozi kupokea zawadi.
Profesa Tibaijuka aliyasema juzi kwenye mkutano wa hadhara na wapiga kura wale uliofanyika kwenye Viwanja vya Red Cross Muleba.
Alisema tuzo hiyo ya heshima ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili na UN ilikuwa ni kwa ajili ya kuthamini mchango wa kazi alizozifanya.
Mbunge huyo alisema kukataa fedha hizo ni kukwepa mtego kama wa mwaka juzi katka suala la Tegeta Escrow ambako alipata mgao wa Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mfanyabiashara wa Kampuni ya VIP.
“Mimi nina marafiki wengi ndani ya nchi na hata nje ya nchi ambao wanapenda kazi zangu ninazofanya na wapo tayari kunichangia.
“Hizo fedha za tuzo wanazosema nimezikataa hazina tofauti na hela za Rugemalira tena zile ni mbaya zaidi,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema tuzo hiyo ilikuwa na vipengele vitatu ambavyo ni cheti, kikombe na dola 100,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 200)
.Alisema alikataa kuzipokea kwa sababu ya sheria za nchi zilivyo sasa kwa viongozi hawaruhusiwi kupokea zawadi.