PATRICIA KIMELEMETA NA AZIZA MASOUD
BARAZA la Maadili ya Utumishi wa Umma limesikiliza shauri la mgawo wa fedha za Escrow dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye anadaiwa amekiuka Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma namba 12 (e) (1) ya mwaka 1995.
Kutokana na madai hayo, waziri huyo wa zamani wa Serikali ya awamu ya nne, amefichua namna alivyotumia fedha za mgawo wa Escrow ikiwamo kutumia Sh milioni 10 kwa ajili ya kununua mboga.
Profesa Tibaijuka alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili jana jijini Dar es Salaam, na kusomewa mashtaka dhidi yake na Mwanasheria wa baraza hilo, Wema Winfred.
Mwanasheria huyo, alidai kuwa Profesa Tibaijuka anakabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuomba fadhila za kiuchumi kinyume na sheria ya maadili kifungu namba 6, kupokea fadhila za kiuchumi kinyume na sheria hiyo na kuwa na mgogoro wa kimasilahi.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alikiuka maadili ya umma kwa kuomba kuingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 kutoka katika Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Tanzania Limited ambazo aliingiziwa kwenye akaunti namba 001200102640201 iliyopo Benki ya Mkombozi, Tawi la St. Joseph jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria huyo alidai kuwa mshtakiwa kwa kutumia wadhifa wake, alijinufaisha kifedha, hivyo baraza linamtaka kueleza bayana mwenendo wake kabla ya hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mbele ya baraza hilo, alisimama mwanasheria wa Profesa Tibaijuka aliyejitambulisha kwa jina la Dk. Rugemaleza Nshara na kupinga tuhuma zinazomkabili mteja wake kwa kudai ameonewa katika shauri hilo.
Kutokana na maelezo ya wakili wa upande wa utetezi, Mwenyekiti wa Baraza, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alimtaka mwanasheria huyo kuelewa kuwa baraza hilo si mahakama ya kisheria, na kwamba taratibu zake hazitofautiani na taratibu za kimahakama.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Msumi aliutaka upande wa walalamikaji ambao ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa ushahidi wao, ambapo aliyekuwa wa kwanza kutoa maelezo yake ni Katibu Msaidizi Idara ya Uongozi wa Siasa wa sekretarieti hiyo, Waziri Kipache (45) aliyedai kuwa anamfahamu mlalamikiwa kuwa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Alisema baada ya kupata taarifa mbalimbali za kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa umma kutuhumiwa kupokea fedha kutoka Kampuni ya VIP kinyume na maadili, alikutana na Tibaijuka na kumhoji kuhusu suala hilo.
“Baada ya taarifa hizo, tulifanya uchunguzi ili tuweze kujiridhisha kama kanuni na taratibu za masharti ya uongozi wa umma yamezingatiwa katika upokeaji wa fedha hizo.
“Tulibaini kuwa Aprili 4, mwaka 2012, Profesa Tibaijuka aliomba fedha kwa mke wa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalila na maombi hayo yaliwasilishwa kwa barua,” alisema Kipeche.
Shahidi huyo ambaye alitoa maelezo yake mbele ya jopo la viongozi wa Baraza la Maadili akitimia dakika kumi, pia alitoa barua ya Profesa Tibaijuka ya kuomba fedha hizo.
Alidai kuwa Profesa Tibaijuka akiwa mmoja wa wadhamini wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust, pia ndiye mmiliki wa Shule ya Kajumulo Alexandre iliyopo mkoani Kagera akiwa ni meneja wa shule hiyo.
“Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, hawaruhusiwi kuomba fedha kwa masilahi ya kiuchumi, hivyo basi Profesa Tibaijuka ametenda kosa hilo,” alisema Kipache.
Kutokana na maelezo hayo ya shahidi huyo, Jaji Msumi, aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi mbele ya baraza kuhusu madai yake hayo.
Kwa kuwa ilikuwa imetimu saa 11: 45, Jaji Msumi aliahirisha shauri hilo hadi mchana kwa kuwa tayari ulikuwa umefika muda wa mapumziko, huku akimtaka Profesa Tibaijuka na timu yake wajipange kwa maelezo na kuwasilisha vielelezo kutokana na tuhuma alizokuwa akituhumiwa.
Ilipotimu saa 6:30 mchana, shauri hilo liliendelea kwa Jaji Msumi kumsimamisha Profesa Tibaijuka atoe ushahidi wake mwenyewe na aeleze namna miamala ya fedha ilivyofanyika.
UTETEZI WA TIBAIJUKA
Akizungumza baada ya madai hayo kutolewa, Profesa Tibaijuka alipinga ushahidi wa Kipeche na kudai kuwa uhusiano wake na taasisi hiyo ni kuwa yeye ni miongoni mwa waanzilishi akiwa na mumewe.
Alisema uamuzi wa kuanzisha shule hiyo, ulitokana na kuona umuhimu wa kupigania elimu ya mtoto wa kike ili aweze kupata fursa ya kuendelezwa kielimu, kiuchumi na kijamii.
Alisema kabla ya hapo alifanya utafiti mwaka 1994 na 1995 ambapo ripoti yake inaonyesha kuwa mtoto wa kike hana thamani kwenye jamii, ndiyo maana anashindwa kupatiwa haki ya kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Profesa Tibaijuka alisema kutokana na utafiti huo, ndipo akafikia uamuzi wa kuanzisha taasisi hiyo ili aweze kuwasaidia watoto hao, hasa wale wenye vipaji na wanaotoka katika mazingira magumu.
“Nikiwa mkereketwa wa Umoja wa Mataifa (UN), sielewi masilahi gani nimepata kupitia fedha hizi, ikiwa shughuli za ‘fund rising’ sijaanza leo, nimeisomea kabisa nchini Marekani kwa fedha za Serikali mwaka 1980.
“Hata nilipokuwa UN nilikuwa nikifanya hivyo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Kofii Annan, aliniruhsu na kunipongeza kuwa ninachokifanya ni muhimu kwa jamii,” alisema Profesa Tibaijuka.
Kutokana na maelezo hayo, aliomba apewe mwongozo nini maana ya kukiuka maadili ya utumishi wa umma, huku akidai kuwa amedhalilishwa, amefedheheshwa na kwamba anaonekana ni tapeli katika jamii, jambo ambalo limemsababishia kukosa amani katika nafsi yake.
“Nimeshangaa kuitwa kwenye baraza hili na kuambiwa kuwa nimekiuka maadili ya utumishi wa umma, kwani maadili maana yake nini? Kufanya shughuli za kuisadia jamii ni kukiuka maadili?
“Ninaomba mwenyekiti unisaidie katika hili ili haki itendeke dhidi yangu, maana nimeanza kuhukumiwa tangu niko bungeni bila hata ya kupewa nafasi ya kusikilizwa, nilijaribu kumwomba Mheshimiwa Spika Anne Makinda ili aweze kunisikiliza, lakini alikataa,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, alilishukuru baraza hilo kumwita na kumsikiliza kwa sababu hajawahi kupata haki yoyote ya kusikilizwa, ndiyo maana alikubali kwenda mwenyewe ili aweze kusema yanayomsibu.
Baada ya maelezo hayo ya Profesa Tibaijuka, walisimama wanasheria watatu wakiongozwa na Getrude Cyriacus, ambaye alikuwa wa kwanza kumuhoji kuhusu malalamiko dhidi yake kuwa aliomba fedha kwa Rugemalila na kuzipokea kupitia Kampuni ya VIP hali ya kuwa maadili hayaruhusu.
Swali hilo lilionekana kuwa mwiba kwa Profesa Tibaijuka, ambaye muda wote alikuwa akisikiliza kwa makini, ambapo alikiri kuomba fedha hizo, lakini si kwa masilahi yake binafsi, bali ni kwa ajili ya Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust.
Wakili Getrude: Wakati unapewa fedha hizo ulikuwa na cheo gani, ni waziri na mbunge au la.
Profesa Tibaijuka: Sioni mantiki ya swali hilo.
Baada ya kujibu, alimwangalia wakili wake, Dk. Nshala ambaye alimtaka alijibu swali hilo, ndipo Tibaijuka alisema kipindi anapokea fedha hizo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Muleba Kusini.
Mwanasheria Hassan Mayunga alimhoji Profesa Tibaijuka kwanini alifanya haraka kutoa fedha hizo zilizoingizwa kwenye akaunti yake katiba Benki ya Mkombozi na kuzitumia katika kazi zake binafsi.
Alisema fedha hizo ziliingizwa tarehe 12 mwaka 2014 na kuanza kufanya miamala binafsi tarehe 14 ambapo Sh milioni mbili alizitumia kununua hisa Makongo Parish.
Profesa Tibaijuka alisema baada ya hapo alitoa Sh 400,000 na kununua hisa Kijiwe Parish na siku hiyohiyo alitoa Sh milioni 10 ambazo hazina maelezo sahihi.
“Sh milioni 10 nilitoa kwa ajili ya kununua mboga kwa sababu fedha hizo ni zangu.
“Nashangaa kuambiwa nimevunja maadili, kwanza fedha hizi ni ndogo japo ni hela, lakini mimi sina shida na fedha hizi.
“Mimi ni mstaafu wa miaka mingi, nina pensheni ya kila mwezi, sina shida na fedha hizo ndiyo maana hata hizo fedha zilizobaki kwenye akaunti hiyo sijaenda kuziangalia kwa sababu sina shida za hivyo,” alisema.
Kabla ya Tibaijuka kuanza kutoa maelezo yake mbele ya baraza hilo, Wakili wa upande wa utetezi, Dk. Rugemaleza Nshala, alisimama na kumuhoji shahidi Kipache na kuzua mabishano.
Dk. Nshala: Kwenye sheria ya maadili wapi inaonyesha kiongozi wa umma kupewa zawadi ni dhambi?
Kipache: Si dhambi ila kisheria inatakiwa isizidi Sh 50,000.
Dk. Nshala: Je, fedha alizopewa Tibaijuka ni zake au za taasisi?
Kipache: Ni za taasisi, lakini tatizo lililopo ni kwamba ameingiziwa fedha katika akaunti yake binafsi na si akaunti ya taasisi na hapo ndiyo amekiuka maadili.
Dk. Nshala: Je, kiongozi wa umma kuomba michango ya maendeleo kwa wadau ni dhambi? Mbona Waziri Mkuu Pinda alikuwa mgeni rasmi kusaidia kukusanya michango ya Taasisi ya Maajar Trust Fund. Je, alikiuka sheria ya maadili?
Kipache: Waziri Mkuu alihamasisha kutoa michango, lakini fedha zilizotolewa hazijaingia katika akaunti yake binafsi, tukio hilo ni tofauti kwa sababu fedha za Tibaijuka aliingiza kwenye akaunti yake binafsi.
Dk. Nshala: Kwanini hawajaenda kwenye bodi ya wadhamini kuuliza kama fedha hizo zimetumikaje au kwenda mbali zaidi kwenye benki ya Mkombozi kuulizia miamala?
Kipache: Hatukuona umuhimu wa kwenda kwa sababu waliokuwa na ‘statement’ ya benki ilionyesha miamala yote iliyofanyika kwa Tibaijuka, lakini pia tulikwenda Rita kufanya uchunguzi ili kuweza kuangalia usajili wa taasisi hii na wamiliki wake.
SHAHIDI WA TIBAIJUKA
Naye shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust, Balozi Paul Rupia, alisema fedha hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka na kutoa taarifa kwenye bodi hiyo kuwa kuna fedha zimeingia ambazo zinatakiwa kulipwa madeni.
Alisema bodi hiyo haijampa masharti yoyote ya kumaliza kulipa madeni hayo na kwamba hawakuwa na sababu ya kumfuatilia kwa sababu walimwamini kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha hizo.
Katika shauri hilo lililoanza saa 3:00 asubuhi na kuendelea hadi saa 11:45 jioni, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya saa tatu kuanzia saa 6:30 mchana hadi saa 9:30 alasiri.
Shauri hilo limehairishwa hadi Machi 13, mwaka huu baada ya wakili wa Profesa Tibaijuka kuomba hudhuru ya kwenda nchini Marekani kwa siku kumi.
Jaji Msumi alikubali ombi hilo na kudai kuwa shauri hilo litaendelea siku hiyo na kutolewa hukumu huku baraza hilo likiamua namna ya kujadili shauri hilo, kwamba itaamuliwa kama liwe la uamuzi wa ndani au hadharani.
Idadi kubwa ya watu walijitokeza katika Ukumbi wa Karimjee kusikiliza shauri hilo.