20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Magadi soda yasigeuke laana Engaruka

Edward Lowassa
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa

NA ELIYA MBONEA, MONDULI

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema hatakubali kuona kiasi kikubwa cha magadi soda kilichogundulika katika Kijiji cha Engaruka Juu, kugeuka kuwa laana kwa wakazi wa eneo hilo. Hivyo aliwataka wakazi na wanavijiji wanaozunguka maeneo hayo kujipanga vizuri kuhusu jinsi ya kujiendesha kwa biashara kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla. Mbunge huyo wa Monduli aliyasema hayo alipofanya ziara ya kazi ya siku moja Jimboni kwake, pamoja na mambo mengine kuzungumza na wakazi wa kijiji hicho kuhusu suala la mradi wa magadi soda, umeme, barabara na maji. Alisema katika siku za hivi karibuni umekuwapo ugomvi kuhusu ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ingawa Umasaini halijazuka tatizo kama hilo. Hata hivyo, aliwaonya wananchi hao kukataa kushawishiwa na watu wachache kuuza maeneo yao kwa tamaa ya fedha lakini hapo baadaye wakajikuta hawana kitu. Alisema baadhi ya watu wameanza kupitapita kwa wananchi kijijini hapo kuwashawishi wawauzie maeneo makubwa ya ardhi jambo ambalo limeibuka baada ya kutambua utajiri mkubwa uliopo katika eneo hilo na manufaa yake baadaye. Lowassa aliwataka wananchi hao kushika walichonacho akisema sehemu ya ardhi ya ekari 29,000 iliyotolewa kwa ajili ya mradi huo wa magadi soda ilitolewa kwa serikali. Alisema kama kutakuwa na watu wanahitaji na kuna ulazima wa kupata basi wanaweza kuingia nao ubia. “Tujipange vizuri kuhusu namna ya kujiendesha kwa biashara kwa manufaa yetu. “Nimekuja na wataalam wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) watueleze ni nini kilichogundulika, kiasi gani, thamani yake na tunafanya nini, na wananchi wa Engeruka wanaweza kufaidikaje. “Mungu ametubariki sana, ametupatia neema kubwa lakini inategemea tutakavyoitumia…inaweza kuwa ni balaa au neema,” alisema huku watu wakisema itakuwa ni neema. Hata hivyo, alikubaliana na wananchi hao kuwa inaweza kuwa neema lakini ikatumiwa na watu wachache na kusababisha kuwa balaa na wao wanakijiji wakabaki hawana kitu, bali wakawa ni watu wa kuzurura barabarani tu. “Hatutaki iwe hivyo ndiyo maana nimekuja hapa na wataalam wa NDC watueleze na ninyi muelewe,” alisema. Akizungumzia kuhusu mradi wa magadi soda, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Mlingi Mkucha, alisema utafiti uliofanywa umebaini kuwapo mita za ujazo trilioni 4.7 za magadi soda katika eneo hilo. Mkucha alisema hali hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu tajiri kwa magadi soda duniani baada ya Marekani na Uturuki. Alisema utafiti umeonyesha kwamba kila mwaka magadi soda yanaongezeka kwa mita za ujazo milioni mbili. Mkurugenzi huyo alisema zitakuwa zikivunwa mita za ujazo milioni moja za magadi soda na hiyo itakuwa kwa miaka 540. Akizungumzia soko la dunia la magadi soda, Mkucha alisema Tanzania itakuwa ikijipatia dola za Marekani bilioni 400 kila mwaka. “Kwa hiyo yatakuwapo mapato yatakayoenda kwenye kijiji, wilaya na mtaona Engaruka itapiga hatua kubwa sana,” alisema. Alisema kwa sasa ni katika hatua ya mwisho kumpata mwekezaji kwa ajili ya kuanza uzalishaji na hadi ifikapo Aprili mwaka huu inatarajia mwekezaji huyo atakuwa amepatikana. Mkucha alisema NDC pia imeanza utafiti wa kuainisha mahitaji ya ardhi kwa ajili ya viwanda mbalimbali vitakavyokuwa vikitumia malighafi hiyo. Alisema utafiti wa maeneo hayo utakuwa shirikishi kwa wananchi wote ili kufikia muafaka wa jambo hilo na ni muhimu wananchi washiriki katika fursa za uzalishaji zitakazojitokeza na siyo kuwa watazamaji. Alisema kinachoangaliwa katika utafiti ni kuona fursa walizonazo wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha mifugo yao ili nao waweze kujikomboa katika uchumi. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Edward Sapuyuni, alisema ekari 9,000 zimewekwa kando kwa ajili ya upanuzi wa viwanda baadaye. Alisema maeneo mengine ya ardhi yatapimwa kwa ajili ya mpango bora wa matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya malisho ili watu au viongozi wasio waaminifu wasipate nafasi ya kuiuza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles