Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MTANDAO wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi, umemwomba Rais Dk. John Magufuli, kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa na Tanzania hasa ile ya usawa wa kijinsia ili kupunguza pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50 katika nafasi za uongozi.
Mikataba hiyo ni pamoja na Mpango Kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Maputo, Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Gender Protocol) na Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binaadamu la mwaka 1948.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP-Mtandao, Lilian Liundi katika taarifa yake aliyotumwa kwa vyombo vya habari, ambapo alisema hiyo ni kwa sababu kumekuwapo na idadi ndogo ya wanawake wanaoteuliwa kuliko ile ya wanaume katika ngazi ya maamuzi.
“Tumefuatilia tangu wakati wa uchaguzi na wakati wa uteuzi wa mawaziri, makatibu wakuu, manaibu na wakuu wa idara na taasisi mbalimbali uliofanywa hivi karibuni na Rais Magufuli.
“Katika uteuzi huo kuna jumla ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu 50 idadi ambayo ni pungufu kidogo ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo walikuwa 53,” alisema.
Alisema idadi ya makatibu wakuu imeongezeka kutoka 23 mwaka 2014 hadi 29 wakati manaibu katibu wakuu imepungua kutoka 30 mwaka 2014 hadi 21 mwaka huu.
Alisema hata hivyo kati ya nafasi zote 50 za walioteuliwa wanawake wapo 10 tu idadi ambayo ni sawa na asilimia 20 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 80.
Alisema idadi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo takwimu za mwaka 2014 zinaonesha walikuwa 20 sawa na asilimia 37.7 huku wanaume wakiwa 33 sawa na asilimia 62.3.