|Susan Uhinga, Muheza
Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS), imepanga kuboresha maeneo yake yenye vivutio vya kitalii ikiwamo Hifadhi ya Misitu Asili ya Amani wilayani Muheza, Tanga.
Mkurugenzi Mkuu wa TFS, Profesa Donsantos Silayo amesema hayo leo alipotembelea Hifadhi ya Misitu Asili Amani wilayani hapa na kujionea changamoto mbalimbali ikiwamo njia za kupita kwenda kwenye kivutio cha maporomoko ya maji.
“Hifadhi ya Misitu Asili ya Amani ambayo ina bustani ya mimea na misitu ya kwanza kwa Afrika imekuwa na vivutio vingi wakiwamo ndwele, imefungua fursa za utalii baada ya muda mrefu kutumika kwa shughuli za mafunzo na utafiti wa ekolojia mbalimbali zilizomo ndani ya Misitu.
“Kutokana na Msitu wa Amani kuwa na vivutio vingi, tumeweka mkakati wa kuboresha miundombinu ikiwamo njia za barabara za kupita watalii kwenda kwenye maeneo ya kuvutia,” amesema Profesa Silayo.
Pamoja na mambo mengine, amesema mkakati huo pia umefungua milango kwa wawekezaji binafsi kuweza kujenga nyumba za kulala wageni ikiwamo usafiri wa kufikisha wageni katika maeneo hayo na watakuwa na wataalamu wenye sifa ya kuelezea kwa ufasaha vivutio vilivyomo humo.
“Tutahakikisha hifadhi hiyo kunakuwa na wataalamu wenye weledi wa utaalamu wa ekolojia ili wageni wanapofika waweze kueleza aina mbalimbali za wadudu, mimea na wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo,” amesema.
Aidha, akielezea idadi ya wageni wanaofika katika hifadhi hiyo Mhifadhi Mkuu wa Amani Mwanaidi Kijazi amesema katika mwaka wa fedha wa 2017-2018 wamefanikiwa kuingiza Sh milioni 59.2 kutokana na wageni 782 waliotembelea hifadhi hiyo.
MWISHO