26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

ZIMBABWE KUANDIKA HISTORIA MPYA

NA MARKUS MPANGALA            |          


WANANCHI wa Zimbabwe wanatarajia kuandika ukurasa mpya wa kisiasa kesho, watakaposhiriki Uchaguzi Mkuu wa kumchagua rais, wabunge na wawakilishi wengine, kama ilivyopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo (ZEC).

Ikumbukwe kuwa, tangu kuasisiwa kwa Zimbabwe mwaka 1980, ni mtu mmoja pekee aliyewahi kushinda uchaguzi kuliongoza Taifa hilo, ambaye ni Robert Mugabe (94). Awali alikuwa waziri mkuu hadi mfumo wa urais ulipoidhinishwa mwaka 1987 nchini humo.

Mugabe, aliyedumu maradakani miaka 37, alilazimika kuondolewa madarakani mwaka jana, baada ya jeshi la nchi hiyo kuingilia kati na kusababisha maandamano ya umma na wafuasi ndani ya chama chake cha ZANU-PF, ambao walianzisha mchakato wa kumpokonya madaraka kwa nguvu.

Wafuasi hao walikasirishwa na kitendo cha Mugabe kutoa nafasi kwa mkewe, Grace Mugabe (53) kurithi kiti cha urais.

Kabla ya mapinduzi hayo ya kijeshi Novemba, mwaka jana, Mugabe alimfuta kazi naibu wake Emmerson Mnangagwa, kwa lengo la kumsogeza karibu mke wake, ili ateuliwe kuichukua nafasi yake.

Hatua ya kwanza ambayo wananchi wa Zimbabwe waliifanya ilikuwa kukubali Emmerson Mnangagwa kuwa mrithi wa kiti cha urais, mabadiliko ambayo yalikuwa ndani ya chama tawala cha ZANU PF, ya pili ni kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu unaoshirikisha vyama vingi vya siasa nchini humo.

Kuondoka kwa Robert Mugabe kumefungua fursa ya watu wengi kuingia katika siasa. Katika kinyang’anyiro cha urais majina 23 yatajumuishwa katika orodha ya wagombea wa urais nchini humo.

Aidha, vyama 55 vya kisiasa pia vinagombea katika uchaguzi wa ubunge. Wadadisi wanasema hili linadhihirisha kuwa, ulikuwapo woga wakati wa utawala wa Mugabe kipindi chote cha miaka 37.

Uchaguzi huo unawahusisha waangalizi wa kimataifa, ikiwamo Jumuiya ya Madola, ambayo imewatuma wawakilishi wao kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 16, kutokana na nchi hiyo kujitoa wakati wa uongozi wa Mugabe.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AfricaNews, limewataja wagombea wenye nguvu hadi sasa katika nafasi ya urais nchini Zimbabwe ni Rais wa sasa Mnangagwa wa ZANU-PF na Nelson Chamisa, anayegombea kwa mwavuli wa Muungano wa upinzani MDC-Alliance, ambao unajumuisha vyama saba vya siasa nchini humo.

Mnangagwa amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi (1980–1988), Waziri wa Sheria na Spika wa Bunge (1988–2005), Makamu wa Rais wa Mugabe (2014 –2017) pamoja na nyadhifa nyingine mbalimbali zilizompandisha chati ya kisiasa.

Mikakati ya mgombea wa chama cha ZANU PF, Mnangagwa ni kuhimiza umoja wa kitaifa, kupambana na rushwa, kuleta maendeleo, kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu, kushirikiana na wananchi, kutengeneza ajira mpya pamoja na kulinda maadili na heshima ya kila mtu.

Kwa upande wake, mgombea wa muungano wa upinzani MDC Alliance, Nelson Chamisa, mwenye umri wa miaka 40, yeye ni mwanasheria na Mbunge wa Kuwadzana. Chamisa alikuwa mtu wa karibu wa aliyekuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC-T, Morgan Tsvangirai, amewahi kuwa Waziri wa Habari mwaka 2009 hadi 2013, wakati nchi hiyo ilipounda serikali ya mseto na Mugabe pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa MDC. Katika muungano wa upinzani wamemjumuisha aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Mseto, Tendai Biti (Peoples’ Democratic Party), mwanasiasa mashuhuri Welshman Ncube (MDC), Jacob Ngarivhume (Transform Zimbabwe), Agrippa Mutambara (Zimbabwe People First), pamoja na vyama vya Multi-Racial Christian Democratic Party na Zanu Ndonga.

Mikakati ya mgombea wa muungano wa upinzani, Chamisa, iwapo akishinda urais ni serikali thabiti, kuimarisha umoja wa kitaifa, mgawanyo sawa wa rasilimali, kuendeleza makazi na miji, kuboresha sekta ya afya, kulinda haki za jamii, kuboresha miundombinu na kuimarisha uchumi.

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria, ikiwa ni mara ya kwanza unafanyika bila kumhusisha Robert Mugabe kama mgombea wa ZANU PF, baada ya miongo mitatu.

Wagombea wengine wanaoshiriki uchaguzi huo ni kiongozi wa Chama cha People’s Rainbow Coalition na makamu wa zamani wa Rais, Joice Mujuru, Busha Joseph Makamba (Free Zim), Chiguvare Tonderai Johann (PPP), Chikanga Evaristo Washington (Rebuild Zimbabwe), Dzapasi Melbah (FMZ), Gaya Mapfumo Peter (UDF), Hlabangana Kwanele (RPZ), Hove Mhambi Divine (NAPD), Kasiyamhuru Blessing  (ZPP),  KhupeThokozani (MDC-T), Madhuku Lovemore (NCA), Mangoma Elton Steers (CD), Manyika Noah Ngoni (BZA), Mariyacha Violet  (UDM), Moyo Nkosana Donald (APA), Mteki Bryn Taurai (Binafsi), MugadzaWilliam Tawonezvi (BCP), Munyanduri Tendai Peter (New-PF), Mutinhiri Ambrose (NPF), Shumba Daniel (UDA) na Wilson Harry Peter (DOP).

Hata hivyo, wakati zikiwa zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi, wanasiasa wa upinzani wameonyesha wasiwasi mwingi kuhusu udanganyifu wa kura dhidi ya kiongozi ya vyama vyao.

“Tume haijaweka wazi taarifa za uchaguzi, hususan matumizi ya vyombo vya habari vya umma na mamlaka, yote hayo yanaonyesha kuwa uchaguzi huu umeanza kugubikwa na udanganyifu. Katika hatua hii, hatujui ni kadi ngapi za kupigia kura zilizochapishwa au wapi zilichapishwa. Kumekuwa na kukataa kwa utaratibu wa viwango vya kimataifa kwa kutoa taarifa ya vifaa vya uchaguzi,” anasema Chamisa.

Chamisa amekosoa kitendo cha chama tawala cha Zanu-PF cha kutoa chakula kwa raia, jambo ambalo alilitafsiriwa kama rushwa kabla ya zoezi la uchaguzi.

Aidha, Chamisa amesisitiza kuwa, katika uchaguzi wa mwaka huu, licha ya changamoto zote wanazokutana nazo, muungano wao hauna mpango wa kususia kwa sababu wana uhakika wa kuibuka na ushindi.

Kwa mara ya kwanza sauti ya waangalizi kutoka nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Madola, ambao wamehudhuria uchaguzi huo wakiongozwa na rais wa zamani wa Ghana, John Dramani Mahama, wamesema Tume ya Uchaguzi, ZEC, kwa mujibu wa sheria, inatakiwa kushirikiana na wadau wa uchaguzi huo kuwa wa kidemokrasia pamoja na kutoa fursa sawa kwa kila chama kushiriki uchaguzi, ikiwamo mchakato wa upigaji kura, uchapishaji wa kura na ulinzi kwa wagombea na wapiga kura.

“Tunafahamu kuwa Zimbabwe inataka kurejesha uanachama wake katika Jumuiya ya Madola. Tunaamini uchaguzi huu utakuwa fursa kubwa ya kuwafanyia tathmini kabla ya kurejeshewa uanachama wao. Jumuiya ya Madola inakuwa mwangalizi wa uchaguzi kwa wanachama wake. Zimbabwe ilikuwa mwanachama na maombi ya serikali yamewadia katika kipindi kizuri, ndiyo maana Katibu Mkuu, Patricia Scotland ametuma waangalizi,” Mahama alisema.

Duru za kisiasa zinasema kuwa, uchaguzi huu ni sehemu muhimu ya kuipambanua Zimbabwe mpya yenye mitazamo mipya ya kidiplomasia pamoja na jumuiya mbalimbali.

Mwaka 2003 Zimbabwe ilijitoa kwenye uanachama wa Jumuiya ya Madola baada ya Mugabe kutuhumiwa na mataifa ya magharibi kuvunja haki za binadamu pamoja na uchaguzi wenye udanganyifu.

Hata hivyo, mwaka huu Rais Mnangagwa aliandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland, kuomba kuridishiwa uanachama wao.

Kwa upande wao, waangalizi wa Umoja wa Afrika, wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemarian Desalegn Boshe, wamesema kuwa, kazi yao ni kutazama taratibu na kanuni zinafuatwa, hivyo hawatajihusisha na suala ka kupigia kampeni upande wowote.

Uchaguzi wa Zimbabwe kama zilivyo chini nyingi za Afrika, masuala ya umasikini, uwekezaji na sera ya umiliki wa ardhi ni miongoni mwa mambo yanayojadiliwa kwenye uchaguzi huu, na ambayo yanatarajiwa kuwa ajenda ya nchi nyingine za Afrika katika chaguzi zake zijazo.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Maendeleo Afrika (AFBD), zinaonyesha kuwa, uchumi wa Zimbabwe ulikua kwa wastani wa asilimia 2.6 mwaka 2017, kutoka asilimia 0.7 ya mwaka 2016. AFDB wameeleza kuwa hatua hiyo ni kufanya vizuri sekta za kilimo, madini, umeme na maji. Kwa mwaka 2018 uchumi wake utategemewa kuongezeka kwa asilimia 1 kutokana na kuathiriwa na masuala ya kisiasa, ikiwamo uchaguzi wa Julai 31, lakini mwaka 2019 unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 1.2, yote hayo yanachangiwa na deni la taifa, uzalishaji hafifu, wawekezaji kukosa imani na changamoto za kisiasa.

Chama tawala kinalaumiwa kwa kushindwa kuwatambua wananchi wa Zimbabwe. Hata hivyo, Rais Mnangagwa amesisitiza kuwa, sera ya ardhi itakayoheshimiwa na serikali yake ni pamoja na kutowanyang’anya wakulima wa kizungu.

Maeneo ya vijijini kama Madzivhe katika Mji wa Beitbridge, wafuasi wa vyama vyote viwili walipambana vikali katika kampeni za mlango kwa mlango. Hata hivyo, wafuasi wa ZANU PF waliwazidi nguvu wale wa MDC Alliance.

Malalamiko hayo pia yameenda kwa mavetarani wa vita nchini humo ambao wanadaiwa kushirikiana na chama tawala kuwatisha watu kwenye nyumba zao ili wakichague chama cha ZANU PF.

Hekaheka za uchaguzi huo zimechochea wanasiasa kutoka vyama vya ZANU PF na MDC Alliance kuwatumia Manabiii ili wawaambie waumini wao kuwa wameonyeshwa na Mungu kwamba chama hicho ndicho kinafaa kuongoza na kuibuka na ushindi.

‘Wanyama wa uchawi’ wapigwa marufuku

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku matumizi tofauti katika nembo za wagombea, kama vile kutumia wanyama, wakiwamo duma, tembo, chui, simba, bundi, swala na faru na risasi – licha ya kwamba bunduki zinaruhusiwa.

Chama tawala Zanu-PF kinatumia picha ya magofu makuu ya Zimbabwe kama nembo yake – jengo la mawe kutoka ufalme wa zamani uliopo kati ya miti miwili inayodhihirisha umoja.

Upinzani MDC ina picha ya mkono ulio wazi kudhihirisha uwazi.

Tunawatakia Wazimbabwe uchaguzi mwema ulio huru na haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles