25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

TFF itafute tiba udhaifu huu wa timu za Tanzania


KWA mara nyingine Tanzania imeendelea kuonyesha unyonge wake katika michuano ya Kombe la SportPesa iliyofikia tamati jijini Dar es Salaam jana.

Unyonge huo unatokana na timu za Simba, Yanga, Singida United na Mbao FC zilizokuwa zinaiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo kushindwa kuibuka na ushindi na kuziacha  timu za Kenya zikiendelea kutawala.

Ifahamike kwamba, mwaka huu ni mara ya tatu kwa michuano ya SportPesa kufanyika, lakini mara zote hizo timu za Tanzania zimekuwa zikiangukia pua.

Michuano ya SportPesa ilianzishwa na kufanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Tanzania mwaka 2017.

Licha ya Tanzania kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo, timu zake hazikumudu ushindani, badala yake timu ya Gor Mahia iliibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa baada ya kuwabwaga ndugu zao wa AFC Leopards katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Taifa.

Mwaka jana michuano hii ilifanyika nchini Kenya, ambako Tanzania iliwakilishwa na timu za Simba, Yanga na Singida United.

Katika michuano hiyo, Gor Mahia iliendeleza ufalme wake baada ya kufanikiwa kuibuka bingwa kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa fainali.

Wakati Simba ilijitutumua na kufika fainali, Yanga na Singida United ziliishia hatua ya kwanza baada ya kuondolewa mashindanoni.

Kwa bahati mbaya, katika michuano ya mwaka huu, mambo ndiyo yameonekana kuwa hovyo kabisa kwa timu za Tanzania, kwani hakuna hata moja iliyofanikiwa kufika fainali.

Badala yake timu za Bandari ya Mombasa iliyoiondoa Simba hatua ya nusu fainali na Kariobangi Sharks, ambayo iliifungashia virago Mbao katika hatua hiyo ndizo  zilizofanikiwa kucheza fainali.

Wawakilishi wengine wa  Tanzania, Yanga na Singida United, wao waliishia hatua ya kwanza tu ya mashindano hayo.

Yanga iliondolewa na Kariobangi Sharks baada ya kuchapwa mabao 2-0, wakati Singida United ilitupwa nje na Bandari, baada ya kufungwa bao 1-0.

Ukiangalia mwenendo huu wa timu za Tanzania katika awamu zote za michuano hii, picha  itakayokujia ni ya kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika ligi yetu ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania, yaani TFF.

Ikumbukwe kwamba, bingwa wa michuano ya SportPesa mbali ya kitita cha fedha anachopata, pia hupata nafasi ya  kucheza mchezo maalumu dhidi ya timu  ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Hatua ya kupata nafasi ya kucheza dhidi ya timu inayoshiriki ligi kubwa duniani inamfanya mchezaji awe karibu na mawakala wakubwa wanaosaka wachezaji.

Na kimsingi timu za Kenya zimekuwa zikiitumia kikamilifu fursa hii kwa kuhakikisha zinaipa umuhimu mkubwa michuano ya SportPesa na hilo linathibitishwa na hatua ya kutwaa ubingwa mara zote tangu michuano hiyo ilipoanzishwa.

MTANZANIA kwa kuliona hilo, tunatoa  wito kwa TFF  kukutana na wadau wake ili kutafuta dawa ya udhaifu huo wa klabu zetu, ili  kuliepusha taifa na aibu nyingine katika michuano ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles