25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Serikali kuongeza kasi mapambano dhidi ya Ukoma

NA VERONICA ROMWALD – MOROGORO

SERIKALI imejipanga  uongeza kasi ya mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa ukoma katika mikoa 10 ambayo bado inakabiliwa na maambukizi.

Imesisitiza itahakikisha inafuatilia kwa karibu misaada yote inayotolewa na serikali kwa kushirikiana na wafadhili kwa watu walioathiriwa na ugonjwa huo, ikiwamo vyakula na vifaa mbalimbali ili iwafikie walengwa.

Hayo yalielezwa mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile.

Alikuwa  akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Chazi, yakiwa na kaulimbiu isemayo ‘Tokomeza  Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma’.

Dk. Ndugulile alisema kuanzia sasa serikali haitasita  kumchukulia hatua mtumishi yeyote atakayebainika kufanya urasimu na kuchepusha misaada inayotolewa kwa waathirika wa ukoma, kinyume na utaratibu uliowekwa.

“Tupo pazuri katika kuutokomeza ukoma, tumekuwa katika mapambano haya kwa miaka 50 sasa, lakini bado tuna changamoto katika mikoa 10 ukiwamo Lindi, Rukwa, Mtwara, Morogoro, Pwani, Tanga, Geita, Dodoma, Tabora na Kigoma,” alisema.

Alisema ili kuongeza nguvu dhidi ya maambukizi ya ukoma, serikali imezindua huduma ya umezeshaji dawa kinga dhidi ya ukoma ikiwa ni jitihada za kuukabili ugonjwa huo.

“Nimeizindua hapa leo (jana), kupitia mpango huu tumelenga kuwakinga watu ambao waliishi au wanaishi kwa ukaribu na watu walioathirika na ugonjwa huu.

“Ukoma ni wa kuambukiza, si ugonjwa wa kurogwa ukoma hausababishwi na kurogwa wala kutupiwa jini.

“Ni vimelea vinaingia mwilini na kusababisha ugonjwa, dawa tunazo za kutosha, hakuna sababu aliyepata maambukizi kushindwa kutibika, vipimo tunavyo vya kutosha, tusiwafungie wagonjwa ndani, wawahishwe hospitalini,” alisema.

Aliwasihi watanzania kujitokeza kumeza dawa kinga  kukingwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao huathiri muhusika na jamii kwa ujumla.

Dk. Ndugulile alishukuru uongozi wa Shirika la lisilo la Serikali la Ujerumani linajishughulisha na mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na Ukoma (GLRA) kwa kushirikiana na serikali bega kwa bega.

Awali, Rais wa GLRA, Patric Miesen alisema Shirika hilo lipo tayari kuendelea kufanya kazi na serikali kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa   nchini.

“Tunasherehekea zaidi ya nusu karne ya kuutokomeza ukoma, nafurahi kumekuwa na mafanikio makubwa Tanzania kupiga vita ukoma hasa kuwawezesha walioathirika na ukoma.

“Hii ni kwa sababu serikali iliona hili ni jukumu lake, bado hatujafika mwisho, lazima tuendelee kupambana dhidi ya ukoma na TB, hadi tuhakikishe hayaleti madhara kwa wananchi,” alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles