24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Hongera Klabu ya Rotari kuwajali walemavu

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SHERIA inayohusu watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 inasema ulemavu ni hali ya kukosa au kushindwa kuwa na fursa ya kushiriki katika maisha ya kawaida ya kijamii kwa kiwango sawa na wengine kwa sababu za kimaumbile, kiakili au sababu za kijamii.

Sheria hiyo inasema mtu mwenye ulemavu ni mtu mwenye udhaifu au upungufu wa viungo, fahamu au akili na ambaye uwezo wake wa utendaji kazi umepungua kutokana na vikwazo vya kimtazamo, kimazingira na kitaasisi.

Aidha, sheria hiyo imetoa wajibu kwa serikali kupitia wizara husika, serikali za mitaa, taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla kutambua na kuzilinda haki za watu wenye ulemavu ili

kutokomeza vitendo vya ubaguzi na vya kikatili dhidi yao.

Kwa sababu hiyo, hatuna budi kuipongeza Serikali, wadau na taasisi mbalimbali zinazoendelea kwa namna moja au nyingine kusaidia, kuwainua watu wenye ulemavu kwa lengo la kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Wikiiliyopita gazeti hili liliandika habari kuhusu moja ya taasisi za kijamii, Klabu ya Rotari ya Dar es Salaam ambayo imetoa msaada wa miguu bandia kwa watu wenye ulemavu 120 wa jiji la Dar es Salaam.

Hao ni wale waliopoteza miguu yao kwa ajali na magonjwa,  hivyo wataweza kutembea tena baada ya kampuni ya Kamal Group kwa kushirikiana na Klabu ya Rotari ya Bahari Dar es Salaam kuwaletea zawadi hiyo ya kudumu ya mwaka mpya.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Mwenyekiti wa Kamal Group, Gagan Gupta, anasema msaada huo umetolewa kupitia mfuko wake wa Uwezeshaji wa Wananchi (Peoples’ Empowerment Foundation – PEF), kwa kushirikiana na Klabu ya Rotari ya Bahari Dar es Salaam.

Anasema bei ya miguu kwa hospitali za rufaa hapa nchini huanzia kati ya Sh milioni 1.2 hadi milioni 3 kwa mguu moja.

Gupta anaeleza kuwa hiyo ni mara ya nne kwa Kampuni ya Kamal kuendesha zoezi kama hili jijini Dar es Salaam, ambapo mpaka sasa imeweza kuwafikia watu wenye ulemavu wapatao 370.

Lengo la msaada huo kwa jamii ya watu wenye ulemavu anasema ni kuwawezesha kupata nguvu na nyenzo za kujitafutia riziki.

“Fursa za kiuchumi kwa watu wenye ulemavu ni chache na jambo hili husababishwa na mambo mbalimbali. Kupitia mradi huu wa viungo bandia, lengo letu ni kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata nguvu na nyenzo za kuwawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi kiurahisi zaidi,” anasema Gupta.

Akizungumzia sababu za kampuni yake kuanzisha mradi huo, Gupta anabainisha kwamba ni baada ya kugundua kwamba mahitaji ya viungo bandia ni makubwa kuliko upatikanaji wake.

Mbali na Gupta, mwakilishi kutoka Klabu ya Rotari ya Bahari Dar es Salaam, Diamond Carvalho, anaeleza kuwa sehemu ya fedha zilizofanikisha msaada huo zimetokana na mchezo wa gofu wa kufunga mwaka wa wadau wa kundi hilo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Klabu ya Rotari ya Bahari Dar es Salaam imetoa jumla ya Sh milioni 23 kufadhili mradi wa viungo bandia kwa mwaka huu.

Carvalho anasema: “Kwa kufanya kazi kwa karibu na PEF, tunaamini tutawafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji wa viungo bandia. Hii inatokana na ukweli kwamba PEF ambayo ni taasisi yenye malengo ya kuwainua wananchi kiuchumi, inamiliki sehemu ya kutengenezea viungo bandia hapa hapa Dar es Salaam ambapo pia inao utaalamu wa kutosha na hupata baadhi ya malighafi hapa hapa nchini,” anasema Carvalho.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 3.6 wenye ulemavu, kati yao, milioni 1.7 wanahitaji viungo bandia.

Takwimu za Chama Cha Walemavu Tanzania (Chawata), zinaonyesha ni asilimia 20 tu ndio wenye uwezo wa kupata viungo bandia, huku wengi wakilazimika kutembelea magongo kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.

Tumalizie makala haya kwa kuipongeza Taasisi ya Rotari Klabu ya Bahari ya Dar es salaam pamoja na Kampuni ya Kamal Group kwa kuona na kujali umuhimu wa jamii ya watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha miguu hiyo ya bandia.

Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya kuwapo sheria inayowatambua watu wenye ulemavu, bado kunahitajika taasisi kama hizi ili kupunguza changamoto zao na baadaye waweze kufikia malengo yao, yakiwamo ya kiuchumi na kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles